
- Na Anne Soy
- Mwandishi Mwandamizi BBC Africa
Chanzo cha picha, Reuters
Afrika italazimika kusubiri “wiki ikiwa sio miezi” kabla ya kupokea chanjo za Covid-19 zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, kulingana na maafisa wanaofanya kazi ya kuhakikisha dozi zinapatikana kwa bara la Afrika.
Karibu dozi milioni 900 zimepatikana hadi sasa kupitia mipango mbalimbali, ya kutosha karibu 30% ya watu bilioni 1.3 wa bara hili mwaka huu.
Kuhodhiwa na mataifa tajiri, upungufu wa ufadhili, kanuni na masharti vimepunguza mchakato wa kuzindua chanjo. “Ulimwengu uko ukingoni mwa kutofaulu kwa maadili na bei italipwa kwa maisha na maisha katika nchi masikini,” alionya mkuu wa WHO Dkt Tedros Ghebreyesus.
Wito wa usawa umekuwa ukiongezeka. Karibu dozi milioni 40 zimetolewa katika nchi zisizopungua 49, zenye kipato cha juu ikilinganishwa na dozi 25 tu zilizotolewa katika nchi moja tu ya kipato cha chini, kulingana na Dk Tedros. “Sio milioni 25, sio 25,000, ni 25 tu,” alisema, bila kusema ni nchi gani.
Kufikia sasa, hakuna chanjo kuu ambayo imeshatolewa barani Afrika, miezi miwili baada ya dozi ya kwanza kutolewa Ulaya.
Muungano wa mashirika na wanaharakati waliopewa jina la Umoja wa Chanjo ya Watu uligundua kuwa “mataifa tajiri yanayowakilisha asilimia 14 tu ya idadi ya watu ulimwenguni walikuwa wamenunua zaidi ya nusu (53%) ya chanjo zote.” Hiyo ilijumuisha chanjo zote za Moderna za 2021 na 96% ya uzalishaji unaotarajiwa wa Pfizer.
Canada iliongoza kwenye chati, kulingana na data na kampuni ya uchambuzi ya Airfinity, “ikiwa na dozi za kutosha za chanjo kwa kila raia wa Canada mara tano”. Mengi ya mahitaji hayo yanapaswa kutimizwa kabla nchi za kipato cha chini kufikiwa.
Barani Afrika, hali hiyo inaamsha kumbukumbu za miaka ya 1990, wakati matibabu ya dawa ya kupunguza makali ya virusi vya ukimwi(ARV) ilipotengenezwa Marekani. Ingawa bara lilikuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa VVU, ilichukua takriban miaka sita kabla ya matibabu ya kuokoa maisha kupatikana kwa Waafrika.
Watu milioni kumi na mbili walikufa barani Afrika kutokana na maradhi yanayohusiana na Ukimwi ndani ya muongo mmoja, pamoja na kupungua kwa vifo nchini Marekani, vkulingana na uchambuzi wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.
Chanzo cha picha, AFP
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAids Winnie Byanyima amekuwa mstari wa mbele kwa wale wanaotaka haki kutoka kwa wazalishaji wa chanjo ya Covid-19.
“Hatumaanishi wapate hasara,” aliiambia BBC. kwa ARV, ilikuwa shinikizo kutoka kwa watu wanaoishi na VVU na wanaharakati wa masuala ya haki ya kuishi ambao walisababisha serikali kuruhusu utengenezaji wa dawa nafuu zaidi kwa kila mtu. ”Gharama ilipungua kutoka $ 10,000 kwa mwaka [kwa kila mtu] hadi $ 100 tu kwa mwaka.”
Anataka njia hiyo hiyo itumike kwa chanjo ya Covid-19, akihimiza soko la dawa “lisiendeshwe kwa nia ya kupata faida maradufu”. Bado wanaweza kupata faida hata kama watashirikisha fomula zao, aliongeza.
Kiongozi wa WHO pia anataka usawa: “Hata wanapozungumza lugha ya ufikiwaji wa usawa, nchi nyingine na kampuni zinaendelea kutanguliza mikataba , kupandisha bei na kujaribu kuwahi mbele ya wengine
Chanzo cha picha, SOPA Images
Kituo cha Covax ni mpango wa WHO na Muungano wa Chanjo ili kusambaza kwa usawa chanjo za Covid-19 ulimwenguni.
“Usambazaji wa chanjo uliagizwa mapema na mataifa tajiri hata kabla ya data ya usalama na ufanisi kupatikana,” alisema Dkt Richard Mihigo, mkuu wa chanjo na maendeleo ya chanjo katika ofisi ya WHO Afrika.
Alipoulizwa kwanini Covax haikufanya vivyo hivyo, alisema kupata fedha ndio kazi ya kwanza ambayo mpango huo ulifanya. Kufikia sasa, dola bilioni sita zimekusanywa kutoka lengo la dola bilioni 8 kwa nchi 92 za kipato cha kati na cha chini, kulingana na Thabani Maphosa wa Muungano wa Chanjo, Gavi.
Kufikia sasa, Covax imepata dozi bilioni mbili kwa kundi hili la nchi, ambayo inajumuisha Afrika yote. Dozi milioni 600 ni kwa ajili ya bara hilo.
Umoja wa Afrika umefanya mipango kwa nchi wanachama kuomba fedha kiasi cha dola bilioni saba kutoka kwa wakopeshaji, ambazo zingegharimia chanjo milioni 270, kwa mujibu wa mwenyekiti wake wa sasa, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Shirika linaloshughulikia watoto la Umoja wa Mataifa, Unicef, ambayo kawaida hushughulika na usambazaji wa chanjo za watoto, itashughulikia vifaa vya kupeleka chanjo za Covid-19 chini ya kituo cha Covax. Wakala unajiandaa kusafirisha angalau mara mbili ya uwezo wake wa kawaida – kile inachokiita “operesheni kubwa na ya kihistoria ya usambazaji”.
Lakini kabla ya kufanyika, nchi zinahitaji kuwa na miundombinu ya kupokea na kusimamia dozi. Benjamin Schreiber, ambaye anaratibu kituo cha Covax cha Unicef, anasema ana “wasiwasi kuwa hatujapata rasilimali na utayarishaji wa kutosha”.
Licha ya mapungufu, anaonesha picha ya matumaini zaidi juu ya uwezo wa bara kuanzisha chanjo mpya. “Afrika ina uzoefu zaidi kuliko maeneo mengine mengi – tumetambulisha kwa wingi chanjo kwa miaka 10 iliyopita na kuna utaalam mzuri wa kuandaa kampeni za chanjo.”
Chanjo moja tu imeidhinishwa na WHO
Lakini hata ikiwa walikuwa tayari, masuala ya udhibiti bado yapo. Chini ya kituo cha Covax, chanjo tu zilizoidhinishwa na WHO zinaweza kununuliwa. Hadi sasa, ni Pfizer tu iliyoorodheshwa kwa matumizi ya dharura na WHO. Mchakato wa kuidhinisha chanjo za Moderna na Astrazeneza unaendelea.
“Chanjo ambazo zinapendekezwa kwa matumizi ya dharura zinahitaji kabisa kufikia viwango vya usalama na ufanisi,” alisema Dk Mihigo.
Nchi zilizoendelea zaidi kama vile Marekani na Mataifa ya Umoja wa Ulaya zina mashirika ya udhibiti ambayo “yanasaidia” kazi ya WHO na kwa hivyo yanaweza kutoa chanjo bila idhini ya chombo hicho. Hatahivyo, nchi nyingi zinazoendelea zinategemea WHO kufanya bidii inayofaa, anaongeza Dk Mihigo.
Uhakikisho huo wa ubora una athari ya moja kwa moja kwa utayari wa watu kupokea chanjo. Utafiti uliofanywa na Africa CDC na Chuo Tiba cha London katika robo ya mwisho ya 2020 iligundua kuwa Waafrika wengi – wanne kati ya kila watano – watakuwa tayari kupata chanjo ya Covid-19 “ikiwa itaonekana salama na madhubuti “.
Nchi kadhaa hata hivyo zimesambaza chanjo ambazo bado hazijaidhinishwa na WHO. “Ushauri wetu ni kwa nchi kutegemea sio tu chombo hicho , lakini pia” Mamlaka ya udhibiti”yoyote yenye uwezo,” alisema Dk Mihigo.
Visiwa vya Ushelisheli, Morocco na Misri zinatoa chanjo ya Sinopharm iliyotengenezwa na Wachina na Guinea, Sputnik V ya Urusi.
Mkurugenzi wa Kituo cha kudhibiti magonjwa Afrika CDC John Nkengasong amesema hakukuwa na mazungumzo yoyote yanayoendelea kuhusu kununua chanjo hizi mbili, lakini kwamba shirika “lilikuwa katika mazungumzo” na nchi zinazozalisha. Nchi zaidi na zaidi za Kiafrika zinaonesha kupendezwa na chanjo hizi mbili wakati wa kusubiri kutoka Magharibi.