Ajali ya ndege Iran: Rais Rouhani awataka wanajeshi kuelezea kilichotokea


Ndege mabaki

Haki miliki ya picha
Getty Images

Image caption

Iran awali ilikanusha vikali taarifa kuwa moja ya makombora yake yaliitungua ndege hiyo.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani amesema kuwa majeshi ya nchi hiyo lazima yaeleze jinsi ilivyodungua kimakosa ndege ya abiria ya Ukraine wiki iliyopita.

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje Mohammad Javad Zarif amekiri kuwa raia wa Iran walidanganywa kwa siku kadhaa baada ya ajali hiyo.

Anasisitiza kuwa yeye na rais hawakufahamishwa kuhusu tukio hilo.

Majeshi ya ulinzi ya Iran yaliwaua watu 176 wakati ilipodungua “kimakosa” ndege ya Ukraine wakati nchi hiyo ilipozozana na Marekani kufuatia mauaji ya jenerali Qasim Solemani.

Saa kadhaa kabla ya ajali hiyo, Iran ilishambulia kwa makombora ya masafa ya mbali vituo viwili vya vikosi vya Marekani nchini Iraq.

Akizungumza katika runinga ya kitaifa siku ya Jumatano, rais Rouhani alitaka jeshi hilo kuangazia hatua ya pili ya uchunguzi “kwa makini”.

“Kitu cha kwanza nikuwaambia watu ukweli. Watu wanaomboleza watafarijika wakijua kwamba tunawawajibisha waliosababisha ajali hiyo kwa kusema nao na kuwaambia ukweli ,” alisema.

Alitoa wito kwa kikosi hicho “kuwaelezea watu kile kilichofanyika tangu ajali hiyo ilipotokea”.

Haki miliki ya picha
Getty Images

Image caption

Wanafunzi wa chuo kikuu ya Tehran wakishikilia picha za waathiriwa wakati wa ibada maalum

Akiwa ziarani nchini India Bw. Zarif, alisema katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni kuwa: “Mimi na rais hatukujua ni [nini kiliangusha ndege hiyo] na punde tulipobaini, tulitoa maelezo”.

Alisifu wanajeshi wa nchi hiyo kwa “kukiri makosa”. Hata hivyo, wakosoaji walishangaa kwanini iliwachukua siku tatu kukira makosa hayo hadi pale mataifa ya magharibi yaliposema yana ushahidi wa kuthibitisha ndege hiyo ilidunguliwa na makombora ya Iran.

Kanda ya video iliyothibitishwa na gazeti la New York Times ilionenesha jinsi makombora yalivyokuwa yakipita katika anga la Tehran na baadae kulipuka ilipokutana na ndege.

Awali ilidhaniwa ndege hiyo iligongwa mara moja lakini baadaye ilibainika kuwa makombora mawili.

Ndege ya Ukraine nambari PS752 ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka mji mkuu wa Tehran, Januari 8, wakati ambapo majeshi ya Iran- yalikuwa yakijiandaa kujipu mashambulio ya kulipiza kisasi kutoka kwa Marekani baada ya kushambulia vituo vyake vya kijeshi nchini Iraq- watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo walifariki.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *