Ali Punjani: Nyumba ya bilionea wa Mombasa yapekuliwa na polisi


Nyumba ya bilionea wa Mombasa Ali Punjani

Polisi wameipekua nyumba ya bilionea Ali Punjani mjini Mombasa. Bwana Punjani anasakwa kuhusiana na uchunguzi wa dawa za kulevya.

Alitajwa kuwa mlanguzi wa mihadarati katika kesi inayoendelea nchini Marekani ambapo watu 4 ikiwemo Wakenya 2 Baktash Akasha na Ibrahim Akasha wanakabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa mihadarati na wanatarajiwa kuhukumiwa Ijumaa ijyo.

Ndugu wa Akasha walikiri kukiuka sheria za mihadarati nchini Marekani ikiwemo njama ya kuingiza kilo 99 za heroin na kilo mbili za methamphetamine nchini Marekani.

Waliwasilisha ombi ambalo wameapa kuwafichua wenzao katika biashara hiyo.

Bwana Punjani mwenyewe anadaiwa kuwa nchini India baada ya familia yake kutoa picha ikimuonyesha kwamba yuko hospitalini.

Anadaiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo. Polisi wamemtaka kujisalimisha.

Tayari maafisa hao wamemkamata mkewe bilionea huyo Bi Karki Sushmi J mwenye umri wa miaka 24 raia wa Nepal aliyekamatwa na raia wengine wawili wanaotoka Nepal na India.

Kamanda wa polisi mjini Mombasa Johnston Ipara amesema kuwa watatu hao walikamatwa kufuatia msako wa nyumba yao siku ya kwanza.

Siku ya Jumatatu zaidi ya maafisa 20 ikiwemo wale wanaokabiliana na mihadarati waliwasili katika makao hayo ya kifahari yaliopo Nyali mwendo wa saa nane mchana.

Maafisa hao waliokuwa wamevalia nguo za raia walilipekua eneo la nyuma ya nyumba hiyo ambalo liko upande wa kuelekea baharini huku mbwa wa kunusa mihadarati wakizunguka magari matatu yaliokuwa yameegeshwa mbele ya nyumba hiyo.

Zaidi ya watu 18 wamekamatwa katika siku chache zilizopita katika operesheni kubwa ya kukabiliana na biashara ya mihadarati mjini Mombasa kufuatia agizo la waziri wa maswala ya ndani Fred Matiangi.

Miongoni mwa wale wanaozuiliwa ni mwanasiasa na maafisa watatu wa polisi.

Maagizo hayo yalitolewa kufuatia uvamizi wa genge la wahalifu kwa jina Wakali Kwanza ambao waliwakatakata wakaazi kwa kutumia mapanga katika eneo la Bamburi huku makumi ya watu wakijeruhiwa.

Waziri huyo wa maswala ya ndani alilaumu kisa hicho kutokana na wauzaji wa mihadarati wanaohusishwa na walanguzi wakuu wa mihadarati na ameapa kufanya msako mkali.

Wakali kwanza ni akina nani?

Kwa mujibu wa Johnston Kipara, kamanda wa polisi mjini Mombasa aliyezungumza na BBC, anasema ni kundi la vijana wahalifu.

‘Lengo lao ni kuweka uoga na kutekeleza uporaji katika jamii’ amefafanua.

Kwa baadhi ya wakaazi, Wakali Kwanza ni moja ya makundi mawili ya uhalifu yanayohudumu katika eneo hilo la pwani na yanafahmika kwa kujihusisha katika biashara haramu na matumizi ya madawa ya kulevya, uporaji na wizi wa mabavu.

‘Jukumu letu ni kuhakikisha mji wa Mombasa unabaki salama na wanaohusika hatua zinachukuliwa wanapopatikana’ amesema kamanda wa polisi Kipara.

‘Inatusaidia kupanga mipango yetu kwa haraka na kuhakikisha kwamba tunakuwa macho kila wakati’ ameongeza.

Mchambuzi wa masuala ya usalama Isaac Mwendwa, anayehusika na kampeni dhidi ya itikadi kali na ugaidi nchini Kenya anasema shambulio la Jumatatu usiku ni ushindani baina ya makundi hasimu ya uhalifu kila moja likitaka kujionyesha nguvu.

Amefafanua kuwa ni kuonyesha ushindani baina ya makundi hasimu yanayotaka kuonekana kuwa na ushawishi katika uhalifu kama biashara ya madawa ya kulevya, wizi na kadhalika.

Tathmini yake ni kwamba serikali haijaonesha kutilia uzito wa kutosha hatari ya inayotokana na magengi hayo japo ni madogo. Amekosoa mbinu inayotumika na maafisa wa utawala anayosema hairidhishi.

Amefafanuwa kwamba kuna haja ya kuwepo jitihada endelevu na za ushirkiano mkubwa wa pamoja na jamii katika Pwani ya Kenya ili kutatua kikamilifu changamoto hiyo na sio tu kwa kuwakamata wahalifu.

Wasiwasi wa jamii

Taarifa zilisambaa kwa kasi na baadhi ya raia waliingia katika mitandao ya kijamii kuelezea wasiwasi na hofu walionayo kutokana na uhalifu wa magengi hayo ya vijana.

Kuna na baadhi waliojipata katikati ya shambulio hilo wakati lililpotokea jana usiku na kutumia mitandao ya kijamiikuelezea kilichowakuta.

Serikali ilitoa makataa kwa wafuasi wa magengi hayo ya uhalifu kujisalimisha.

Aliyekuwa mkuu wa polisi katika kaunti hiyo Nelson Marwa, amesema makundi hayo ya vijana hufadhiliwa na baadhi ya matajiri wenye ushawishi katika eneo hilo la pwani.

Uchunguzi sasa unaangazia kwanini yamefanyika, na uhalifu ulitekelezwa kwa ushirikiano wa nani.

Maswali ambayo pia yameulizwa na baadhi katika mitandao ya kijamii, kwamba dhamira ya mashambulio hayo dhidi ya Wakenya wasiokuwa na hatia ni ipi? na ni nani mfadhili wa makundi hayo?Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *