'Baba alinifunza kunywa pombe na kuvuta sigara'


Anne Njeri Mathu

Image caption

Anne Njeri Mathu dada aliyefunzwa na baba yake kunywa pombe

Harufu ya pombe tu ndio ilikuwa kivutio kikuu kwake Anne Njeri Mathu kwa miaka mingi.

Shughuli zote za siku kwake alizipanga kwa kutegemea ni vipi angeweza kubugia pombe wakati wowote, iwe mchana au usiku.

Alikuwa ni mraibu wa pombe na hakuwa na aibu hata kidogo kuhusu hilo.

Je mara yake ya kwanza kuonja pombe ni lini?

Anne anasema alikuwa na miaka 10 pekee, wakati baba yake mzazi alipompa pombe aonje, na ikawa ni desturi kuwa kila mara baba yake alipokuwa anakunywa mvinyo angempa kionjo. Anne anasema kuwa wakati huo alihisi pombe ikiwa tamu na hakuona ubaya wa kuibugia kwa kuwa baba yake mzazi alimuonyesha jinsi ya kuinywa.

Baba yake alikuwa na uzoefu wa kunywa vileo wakati alipokuwa anapumzika nyumbani, pia Anne ana kumbukumbu kuwa ni baba yake aliyemfunza jinsi ya kuvuta sigara.

“Mara ya kwanza aliniomba nimsaidie kuwasha sigara, kisha akaniambia nifanye kama napumua moshi huo uingie ndani yangu, nilipokohoa akaniambia niendelee kuvuta ili kikohozi kiishe.”

Na kwa hivyo alipofika kidato cha tatu alikuwa ni mraibu wa kunywa pombe na kuvuta sigara.

Anne anakumbuka akiwa shule ya sekondari alikuwa anabeba vileo pamoja na mahitaji mengine ya shuleni, kuhakikisha kwamba anakata kiu ya pombe.

Maisha ya mama huyu ambaye sasa ana umri wa maka 56 anayataja kuwa na kukurukakara za kila aina.

Anne Njeri Mathu kutoka nchini Kenya wakati mmoja alikuwa anawania taji la kuwa mlimbwende nchini humo.

Miaka ya 80 alikuwa miongoni mwa wanawake waliorodheshwa kuwa warembo zaidi nchini Kenya ila alikuwa pia anafahamu kwamba tayari ametekwa kwenye uraibu wa pombe.

“Nilikuwa maarufu sana nikiwa kwenye taasisi ya Nairobi Polytechnic. Nilikuwa napokea mialiko ya kwenda sherehe mbalimbali. Maisha yangu yalizungukia katika vilabu na maeneo ya burudani. Masomo hayakuniingia akilini, nilipenda anasa sana,” anasema.

Anne anasema kuwa kutokana na tabia hizo pamoja na unywaji pombe wa kupindukia alifeli mitihani ya taasisi.

Image caption

Anne alikuwa tayari kutoroka kazini akajifiche mahali apate hata kama ni pafu tu la pombe ndio kazi ifanyike

Kupata kazi kisha kuipoteza

Mwaka wa 1983, alipata kazi yake ya kwanza katika shule ya sekondari ambapo alikuwa msimamizi wa upishi. Ni wakati huo huo pia alipojaliwa mtoto wake wa kwanza.

Anne anasema wakati huo eneo alilokua anafanyia kazi lilikuwa karibu na kambi ya jeshi, kwa hivyo ilikuwa rahisi kupata vileo kwa bei nafuu.

Ni wakati huo ambapo kiu yake ya pombe ni kama ilipanda maradufu. Kwa kuwa alikuwa anafanya kazi katika mazingira ya shule, ujanja wake uligundulika na akachishwa kazi kwa sababu ya ulevi .

“Nilikuwa na bahati kwani nilifanikiwa kuajiriwa katika hoteli moja ya kifahari jijini Nairobi. Kama kawaida mazingira ya hoteli nyingi uuzaji wa pombe kwa wingi i jambo la kawaida. Niliendeleza uraibu wangu wa ulevi,” Anne anakumbuka.

Akiwa kazini hotelini anasema ilimlazimu mara nyingi kunywa pombe ilimradi mwili wake uweze kufanya kazi, kwa kuwa kama hajabugia kinywaji, alikuwa anapata shida kwelikweli. Alikuwa anatetemeka na kujihisi kama mwenye homa kali.

Alianza desturi ya kunywa pombe kama kiamsha kinywa asubuhi na mapema ili kuepukana na dalili hizo.

Anakiri kukwepa kazi hata masaa ya mchana almuradi apate wasaa wa kenda kunywa pombe aliyokuwa anaificha kwenye vyumba ambavyo havikuwa na wateja. Wasimamizi wa hoteli hiyo walijaribu kumsaidia na hata kumhamisha katika hoteli nyingine mbali na jiji.

Lakini ilikuwa vigumu kwa Anne kuacha pombe. Mwishowe aligombana na wasimamizi kuhusiana na ulevi wake na akaamua kuacha kazi.

Pombe iliharibu ndoa!

Anne alikutana na mume wake wa kwanza mwaka wa 1994.

Alikuwa daktari na pia mlevi mwenzake. Miaka mitano baada ya ndoa mumewe aliaga dunia kutokana matatizo ya kiafya yaliyobabishwa na unywaji pombe kupindukia.

Anne anasema kuwa mara ya mwisho kumuona mumewe huyo akiwa hai walikuwa walevi na alianza kutapika damu na katika kipindi cha saa moja tu, alifariki dunia.

“Mashemeji wangu walinilaumu kutokana na kifo chake. Walitwaa vitu vyote vya thamani tulivyomiliki na kuniacha maskini,” Anne anasema.

Alianza kuishi na rafiki yake mmoja huku mama yake mzazi akichukua jukumu la kuwalea watoto wake wawili.

Wakati huo alikuwa hana fedha, wala ajira kwa hivyo aligeukia vinywaji vya bei ya chini kukidhi hamu yake ya kunywa pombe.

Ni wakati huo ambapo rafiki yake mmoja aliyekuwa anaishi Ujerumani alipoona hali yake akaamua kumsaidia kubadilisha mazingira alimokuwa anaishi.

Rafiki yake alimsaidia kusafiri hadi ujerumani kama njia ya ‘kumtenganisha’ na pombe, ila hakufahamu kuwa ndio mwanzo ukoko ulikuwa unaalika maua.

“Nilipofika Ujerumani, nilikutana na mwanamume mwenye asili ya Kijerumani. Yeye pia alikuwa na uraibu wa pombe japo alikuwa mkongwe mwenye umri wa zaidi ya miaka 70,” Anne anakumbuka. Baadaye walifunga ndoa.

Wakati huo Anne na mume wake mpya walikuwa kazi yao ni kunywa mchana kutwa.

Anne anakiri hakuwa na mapenzi kwa mume huyo ila tu alikuwa amekutana na mtu ambaye wangesaidiana katika uraibu wake wa pombe na mwanamume mwenyewe hakuwa na matatizo ya kifedha.

Lakini baada ya muda yule mume wake pia hakuweza kuhimili kasi ya ulevi na hatimaye baada ya miezi kadhaa aliaga dunia.

Ilibidi arejee nchini Kenya ambapo alianza kwa kuuza kila kitu alichokuwa nacho katika juhudi za kufanikisha ulevi wake.

Maisha yalidorora mno kiasi kuwa Anne alihisi kana kwamba kifo kinamwandama. Hii ni kutokana na kwamba alikuwa hawezi kufanya chochote bila kunywa.

Image caption

Anne alivyokuwa amedhoofika kutokana na ulevi wa kupindukia

Alivyoanza kunywa pombe za rejareja

Uliwadia wakati ambapo alikunywa pombe aina yeyote mradi alewe tu, kuanzia pombe kali iliyoharamishwa nchini Kenya ya changa’aa hadi busaa.

Swahiba wake wa karibu alikuwa ni ndugu yake kwani walikuwa wanakunywa pamoja kila wakati.

“Niligundua aina ya pombe kwa jina mandege au jeti nadhani ilikuwa inatumika kama kemikali katika maeneo ya viwandani. Ilikuwa inauzwa kwa watu kama sisi ambao walihitaji kulewa kwa haraka bila kujali. Mimi na ndugu yangu tulihisi kana kwamba tumepata njia rahisi ya kulewa.”

Anne anakumbuka siku moja ya Jumapili alipoamka akiwa na lengo la kwenda kanisani. Alihisi kana kwamba alihitaji Mwenyezi Mungu, ili kumtoa kwenye lindi la ulevi.

Anasema alipofika kwenye lango la kanisa, waelekezi wa waumini walimzuia kuingia wakishangaa alikuwa amekunywa nini.

Kutokana na kule kukejeliwa katika eneo alilodhani angepata usaidizi Anne alijaribu kujitoa uhai kwa kumeza tembe nyingi kwa mpigo.

Kwa bahati, nduguye alimuokoa kwa wakati na kumpeleka hospitalini.

Haikuchukua muda kwa Anne kukubali kupelekwa katika kituo kinacho wahudumia watu wenye uraibu wa pombe na dawa za kulevya.

Alikaa kituoni kwa siku 90. Anasema haikuwa safari rahisi kwani alikuwa na matatizo ya kula kutokana na kudhoofika kwa mwili wake uliokuwa umezoea pombe kama chakula. Anasema kwamba chakula chake kilisagwa kama cha mtoto mdogo ilikipite kooni.

Baada ya miezi mitatu Anne alikubali kwamba alikuwa taabani na hapo ndipo alilivalia njuga swala la kubadilika kabisa.

Alianza maisha upya na hatua moja baada ya nyengine alisahau pombe na kugeukia kuwa mtoa nasaha dhidi ya ulevi.

Hiyo ndiyo kazi anayoifanya hadi sasa.

Je maisha yamekuwaje baada ya mabadiliko hayo?

Anne anakiri imekuwa pandashuka lakini yenye kuzaa matunda mazuri.

Kwa mfano alianza mpango wa kuwasaidia watu ambao wametekwa na pombe na dawa za kulevya, kwa jina ‘Sober Again Outreach’

“Mimi ninaweza kuelewa wanachohisi watu walevi na kwa hivyo ninachukua jukumu la kuwasaidia kuachana na ulevi.”

Pia Anne aliandika kitabu ambacho sasa amekichapisha kwa jina ‘Sober Again’.

Anasema kuwa ilimchukua muda wa mwaka mmoja kuandika kitabu hicho kwa kuwa ilihitaji kurudisha mawazo nyuma ili kufufua kumbukumbu ya maisha ya ulevi ambayo nusra yampeleke kaburini.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *