Chadema yataka Lissu ahakikishiwe usalama wake kabla ya kurejea Tanzania


Tundu Lissu ambaye alinusurika jaribio la kuuawa miaka miwili iliyopita, amesema hayuko tayari kurudi nyumbani na ataendelea kubakia ughaibuni hadi pale atakapohakikishiwa na Serikali ya Tanzania yu salama.

Chama kikuu cha upinzani nchini humo, Chadema kimesema kinaafikiana na uamuzi wa Tundu Lissu kikisema kuwa yale yaliyomkumba miaka miwili iliyopita wakati akireja kwenye maskani yake akitokea katika vikao vya bunge bado yanaendelea kujitokeza hadi sasa.

Chama hicho kimesema jaribio la mbunge huyo kurejea nyumbani kama alivyokuwa ameahidi hapo awali kuwa angerejea mwezi uliopita lilisitishwa hasa baada ya kujitokeza baadhi ya watu wakimtishia kumdhuru  wakati anaporejea nyumbani.

Mkurugenzi wa itifaki, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa chama hicho, John Mrema amesema ingawa mwanasiasa huyo haijulikani ni lini atarejea lakini amesisitiza kuwa suala la usalama wake ndiyo linalopewa kipaumbele kwa sasa.

Lissu asema hakusudii kurejea nyumbani kwa sababu za kiusalama

Tundu Lissu aliyevuliwa ubunge hivi karibuni, amekuwa akiishi nchini Ubelgiji tangu aliponusurika katika jaribio la kuuwawa miaka miwili iliyopita, na mara kadhaa amekuwa akifanya ziara katika mataifa ya Magharibi ambako pamoja na mambo mengine hufanya mahojiano na baadhi ya mashirika ya kimataifa.

Akizungumza na shirika la habari VOA nchini Marekani, mwanasiasa huyo alisema ingawa sababu za kiafya za kuendelea kukaa nchini Ubelgiji haziko tena, lakini hakusudii kurejea nyumbani kwa sababu za kiusalama.

Awali mwanasiasa huyo ambaye wakati fulani alidokeza ndoto yake ya kutaka kuwania urais katika uchaguzi wa mwakani, alisema angerejea nyumbani Septemba 7, akiksisitiza atarejea mchana kweupe.

Mwandishi: George Njogopa

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *