Kanisa Anglikana Kenya lapiga marufuku siasa madhabahuni


Kanisa la Kianglikana nchini Kenya limepiga marufuku wanasiasa kuhutubia waumini kwenye madhabahu. Askofu mkuu wa kanisa hilo Jackson Ole Sapit amesema wanasiasa hutumia madhabahu kuligawanya taifa na kuwakejeli wapinzani wao. Hayo yanajiri wakati kanisa hilo likipiga marufuku michango ya wanasiasa. 

“Hatutaruhusu madhabahu kuwa mahali pa kupigia siasa, iwapo tutawaruhusu wanasiasa kuzungumza na washirika, watafanyia tu kule nje baada ya ibada, tunataka kusikia neno la Mungu sio siasa.” Ole Sapit amesema.

Kanisa liko njia panda, kwa miaka na mikaka, wanasiasa wamekuwa wakitumia rasilimali zao kuchangia kwenye miradi ya kanisa, kwani baadhi yao ni washirika. Kwa wengi kanisa limepakwa tope na wanasiasa ambao hutumia madhabahu kwa maslahi yao wenyewe. Lakini sasa Askofu Mkuu wa kanisa la Kianglikana, Joseph Ole Sapit anajaribu kulisafisha.

Sio mara ya kwanza kwa wanasiasa kusuluhishia tofauti zao kwenye madhabahu. Jumapili iliyopita ibada katika kanisa moja la Kianglikana lililoko katika jimbo la Kiambu ilisitishwa baada ya mwanasiasa mmoja kuanza kumtusi mpinzani wake alipopatiwa nafasi ya kuwasalimu waumini. Waumini walianza kumzomea hadi ibada ikasitishwa.

Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa akizungumza ndani ya kanisa la Kianglikana All Saints Cathedral jijini Nairobi Oktoba 5, 2017

Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa akizungumza ndani ya kanisa la Kianglikana All Saints Cathedral jijini Nairobi Oktoba 5, 2017

Hatua ya Kanisa hilo la Kianglikana, inajiri miezi michache tu baada ya kupiga marufuku, michango ya wanasiasa kanisani humo. Ole Sapit amewakosoa wanasiasa ambao hutumia pesa zao kama chambo cha kutumia madhabahu. Mkurugenzi Mkuu wa mashtaka Noordin Haji anasema baadhi ya wanasiasa hutoa fedha haramu kanisani.

“Kama viongozi wa dini na taasisi, mna haki ya kukataa fedha ambazo hamfahamu zinapotoka, mna uwezo wa kujenga asasi za kutambua vyanzo vya fedha zile na kama hamna uwezo huo, basi sisi tupo tutawasaidieni.” Amesema Noordin Haji.

Sapit amesema ataendelea kuwahamasisha waumini jinsi ya kukabiliana na ufisadi. Baadhi ya wakenya wanasema kuwa kanisa ndilo kizingiti kikuu cha vita dhidi ya ufisadi huku likiendelea kupokea mamilioni ya fedha kutoka kwa wanasiasa waliopotoka kwa ajili ya kukamilisha miradi yake.

Kanisa la Kianglikana nchini Kenya linajiunga na kanisa Katoliki ambalo huwa haliruhusu wanasiasa kupiga siasa ndani ya kanisa, je makanisa mengine yatafuata mkondo huo?Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *