Kenya na Tanzania zaongoza kwa idadi ya mabilionea Afrika mashariki


Kenya na Tanzania zinaongoza kwa idadi ya watu matajiri katika jumuiya ya Afrika mashariki kulingana na utafiti.

Kulingana na ripoti ya 2019 kuhusu utajiri barani Afrika iliochapishwa mwezi Septemba na benki ya AfrAsia, Kenya inaongoza ikiwa na mabilionea 356, Ikifuatiwa na Tanzania ambayo ina mabilionea 99.

Uganda ni ya tatu ikiwa na matajiri 67 huku Rwanda ikifunga orodha hiyo na mabilionea 30.

Ripoti hiyo inasema kwamba matajiri hao wana utajiri wa dola bilioni 10 na kwamba Tanzania ina tajiri mmoja wa dola bilioni moja.

Barani Afrika ripoti hiyo inasema kwamba Afrika Kusini inaongoza kwa matajiri ikiwa na mabilionea 2,169, Misri 932 na Nigeria 531.

Hatahivyo ripoti hiyo haitaji hata bilionea mmoja mbali na mali anayomiliki.

Katika miji mikuu, mji wa Nairobi unaongoza ukiwa na utajiri wa dola bilioni 49 mbele ya mji wa Dar es salaam ambao umeorodheshwa wa 11 na una utajiri wa dola bilioni 24.

Mji mkuu wa Uganda Kampala una utajiri wa dola bilioni 16 huku Addis Ababa ikiwa na utajiri wa dola bilioni 14.

Mtu tajiri zaidi barani Afrika ni mfanyabiashara Aliko dangote kutoka Nigeria

Kulingana na ripoti hiyo mabilionea wa Afrika ni asilimia 16 pekee ya idadi ya mabilionea wote duniani, huku Afrika ikiwa na silimia moja pekee ya utajiri wote duniani.

Utajiri unaomilikiwa na bara hilo ni dola trilioni 2.2 kwa jumla ambapo asilimia 42 ya utajiri huo unalimikiwa na watu wenye utajiri wa kiwango cha juu au HNWIs.

Kwa ujumla mtu mwenye mapato ya kiwango cha kadri anayeishi Afrika ana mali inayogharimu dola 1,900.

Ripoti hiyo inasema kwamba kuna matajiri 140,000 wanaoishi barani Afrika kila mmoja wao akiwa na mali yenye thamani ya dola milioni 10.

Vilevile kwa mujibu wa ripoti hiyo kuna takriban mamilionea 6,900 wanaoishi Afrika kila mmoja akiwa na mali yenye thamani ya dola milioni 10 ama zaidi mbali na mabilionea 23 kila mmoja wao akiwa na mali yenye thamani ya dola bilioni moja.

Bilionea mwenye umri mdogo zaidi Afrika

Mo Dewji

Haki miliki ya picha
AFP/Getty Images

Mohammed Dewji, maarufu kama Mo Dewji, ni mmoja wa wafanyabiashara wanaofahamika sana kutoka nchini Tanzania.

Ni bilionea ambaye ametambuliwa kuwa miongoni mwa mabilionea wa umri mdogo zaidi Afrika.

Dangote: Nikiinunua Arsenal nitamfuta Wenger

Ni mfanyabiashara na mwanasiasa ambaye pia amewekeza katika kandanda na pia katika shughuli za hisani. Ni mnyenyekevu na huwa mara nyingi haandamani na walinzi kama ilivyo kwa wau mashuhuri.

Alipokuwa anatwekwa eneo la Oyster Bay alikuwa anajiendeshea gari mwenyewe.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda aligusia hilo akizungumzia hali ya usalama Dar es Salaam: “Na ndio maana hata Mo mwenyewe angeweza kuwa na mabodyguard (walinzi) lakini kwa sababu ya amani iliyoko katika mkoa wetu, anatembea peke yake.”

Mo Dewji ni nani?

Mo alizaliwa tarehe 8 Mei mwaka 1975, ikiwa na maana kwamba kwa sasa ana miaka 43.

Alizaliwa eneo la Ipembe, Singida maeneo ya katikati mwa Tanzania.

Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, ana utajiri wa dola bilioni 1.5.

Ni wa pili miongoni mwa watoto sita wa Gulamabbas Dewji na Zubeda Dewji.

Alisomea elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Arusha na baadaye akasomea elimu ya sekondari katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam.

Alihamishiwa Marekani kwa masomo zaidi ya sekondari katika jimbo la Florida mwaka 1992.

Alisomea chuo kikuu cha Gerogetown jijini Washington DC na kuhitimu mwaka 1998 akiwa na shahada ya kwanza katika biashara ya kimataifa na fedha, na masuala pia ya dini. Miongoni mwa watu mashuhuri waliosomea chuo kikuu hicho ni rais Bill Clinton, rais wa zamani wa Ufilipino Gloria Arroyo, Mfalme wa Jordan Abdullah na wachezaji wa NBA kama vile Allen Iverson na Patrick Ewing.

Baada ya kufuzu, alirejea Tanzania na kuanza kushiriki katika usimamizi wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) iliyoanzishwa na babake miaka ya 1970.

Image caption

Fedha

Alihudumu kwa miaka miwili kabla ya kuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo, wadhifa ambao ameendelea kuushikilia hadi sasa.

Mo ndiye tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia miongoni mwa matajiri wa umri mdogo zaidi Afrika.

Kampuni ya METL, kwa mujibu wa Forbes, ilifanikiwa kwa kununua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti.

METL ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.

Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.

Kwa mujibu wa tovuti yake, METL inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.

Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

METL ina shughuli zake katika nyingi barani Afrika na ina malengo ya kujipanua zaidi katika maeneo zaidi.

Inaendesha shughuli zake Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Malawi, Msumbiji na Zambia, ambapo huajiri watu zaidi ya 28,000.

Haki miliki ya picha
AFP

Shughuli za MeTL huchagia 3.5% ya jumla ya pato la taifa (GDP) la Tanzania.

Kiwango cha wastani cha ukuaji wa mapato ya kampuni hiyo kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2014 kutoka $30 milioni hadi $1.3 bilioni kilikuwa ni 200%.

Lengo la kampuni hiyo ni kuongeza mapato ya taifa lake hadi $5bn kufikia mwaka 2020, pamoja na kuwaajiri watu 100,000.

Mo Dewji ameorodheshwa wa 17 kwenye orodha ya mabilionea barani Afrika na wa 1561 duniani kwenye orodha ya mabilionea mwaka 2018.

Wakati mmoja kampuni yake ilianzisha Mo Cola kushindana na Coca Cola.

Wakfu wa hisani

Dewji ni Mtanzania pekee aliyesaini mkataba mwaka 2016 wa kutoa kwa wahitaji nusu ya mali yake.

Mo Dewji Foundation ndio asasi ambayo aliianzisha mwaka 2014 ili kutekeleza nia yake hiyo na kazi yake kubwa ni kusaidia watanzania wasiojiweza kwa upande wa afya, elimu na maendeleo jamii.

Kujiingiza katika siasa

Mbali na biashara na shughuli za jamii Mo Dewji amewahi kuwa mwanasiasa na mwaka 2005 mpaka 2015, Mohamed Dewji alikuwa mbunge wa Singida Mjini.

Alijiingiza katika siasa mara ya kwanza mwaka 2000 ambapo alishinda uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika eneo hilo, wakati huo akiwa na miaka 25, lakini akazuiwa kuwania kwa madai kwamba alikuwa bado mdogo wa umri.

Alistaafu kutoka kwenye siasa baada ya kuhudumu mihula miwili.

Tuzo

Mwaka 2012, alitawazwa Kiongozi Mdogo Duniani kwa Kiingereza Young Global Leader (YGL) wakati wa kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa uchumi Duniani (WEF).

Mwaka 2015, alitajwa kuwa bilionea wa umri mdogo zaidi Afrika na jarida la Forbes na baadaye akatawazwa Mtu Mashuhuri wa Mwaka wa Forbes.

Mwaka uliopita, alishinda tuzo ya Afisa Mkuu Mtendaji bora wa Mwaka Afrika katika mkutano mkuu wa maafisa wakuu watendaji wa Afrika.

Familia: Mke wake na watoto

Mke wa Dewji huitwa Saira, aliyekuwa wanapendana tangu utotoni, na wamejaliwa watoto watatu Nyla, Abbas na Mahdi. Alifunga ndoa mwaka 2001. Mo na mke wake walikutana Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam.

Klabu ya Simba SC

Dewji pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba Sports Club inayocheza katika Ligi Kuu ya Tanzania ambapo ni mfadhili mkuu kwa sasa.

Amekuwa akifadhili ujenzi wa uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo.

Haki miliki ya picha
AFP/Getty Images

Sababu ya kurejea Tanzania kutoka Marekani

Mo Dewji alisomea Marekani na mpango wake ulikuwa kusalia na kufanya kazi huko.

Ilikuwaje mwishowe akajipata Tanzania?

Mwezi Septemba, aliandika kwenye Instagram sababu iliyomfanya kurejea, ambapo anasema ni ushauri wa babake pamoja na kugundua kwamba kulikuwa na fursa nyingi Tanzania.

Ujumbe aliouandika 10 Septemba, 2018 ndio huu:

“Nilipomaliza masomo yangu ya shahada nikiwa nchini Marekani niliamua kubaki huko na kufanya kazi. Nilitumia muda na nguvu nyingi kazini lakini pesa ambayo niliipata haikukidhi kufanikisha malengo yangu.

“Ndipo Baba yangu akanishauri nirejee nyumbani Tanzania na nilipofatilia kwa kipindi hicho niligundua kwamba Tanzania kuna fursa nyingi za kibiashara na hapo ndipo nilipoamua kurudi na kujiunga katika biashara ya familia.

Muhimu kufahamu ni kwamba mafanikio sio lazima uende kuyatafuta nje ya nchi, hapa hapa nchini kwetu kuna fursa ambazo ukifanyia kazi utafanikiwa. Unafikiri kwanini baadhi ya watu wanapenda kuishi/kufanya kazi nje ya nchi?”

Nukuu muhimu za Mo Dewji

Mara kwa mara, hutoa ushauri, na pia huwa hafichi upendo wake kwa klabu ya Simba FC ambayo ndiye mdhamini wake mkuu.

  1. Ijumaa wiki iliyopita, aliandika: “Kila jambo unaloogopa, Mungu ana mpango wake. Mungu ni mkuu kuliko hofu uliyonayo. Ana mamlaka na maisha yako ya baadae. Kuwa na imani.”
  2. Kuhusu urafiki na mikopo, kauli yake hii: “Hamna kitu kinaua urafiki kama mikopo!”
  3. Kuhusu utajiri na umaskini, aliweka nukuu hii aliyoitoa kwingine pengine kwenye Twitter majuzi: “Walio fukara hujaribiwa kwa umaskini, sisi nao hujaribiwa kwa kupewa zaidi ya tunavyovihitaji.”
  4. Ana ushauri pia kuhusu kufanikiwa maishani: “Vitu vingi katika maisha vinaweza kujaribu kukuondoa kwenye malengo yako lakini usipoteze mwelekeo. Mipango inaweza kubadilika lakini kamwe sio mwisho wa safari!”
  5. Kuhusu kuwezeshwa kwa wanawake: “Kwenye Uislamu, mwanamke hahitaji kuwezeshwa na mwanaume, wameshawezeshwa na Mungu.”
  6. Kuhusu kuwa mfano bora kwa watoto: “Mtoto wako atafata mifano yako, sio ushauri wako. Hata tunapofikiri hawatuoni, wanatuona. Hata tunapofikiri hatulei, tunalea.”Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *