Kenya: Polisi yabaini genge la wahalifu linalowadanganya wasichana kwa njia ya mtandao


Police patrol in Nairobi, Kenya

Maelezo ya picha,

Polisi mjini Nairobi imepata wasichana watatu ambao walisemekana hawajulikani walipo

Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI nchini Kenya, inachunguza “genge la mtandaoni” ambalo linalenga wasichana wa shule waliokwama majumbani kwasababu ya virusi vya corona na kuwashawishi katika kile maafisa wanakielezea ni kuwadanganya na kuwapotosha kimaadili.

Hayo yanawadia baada ya wasichana watatu vijana waliokuwa wamepotea kuokolewa na maafisa wa polisi mjini Nairobi.

Watatu hao wamewaambia polisi kuwa waliona akaunti kwenye mtandao wa kijamii unaowaalika katika tafrija au sherehe mjini Nairobi.

Aidha, polisi imewataka wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao kwa karibu.

Ofisi ya idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), ingependa kuwafahamisha kuwa tunawatafuta wafuasi wa genge hilo na watakamatwa kujibu maswali ya uhalifu wao,” Idara hiyo ya polisi imesema kupitia mtandao wa Twitter.

Visa vya wasichana wadogo kupotea vimejitokeza sana siku za hivi karibuni baadhi wakisema waliahidiwa kazi.

Mapema wiki hii jamaa ya msichana mmoja aliweka ujumbe wa kusikitisha katika mtandao wa Twitter akihofia kuwa pengine msichana wao ametekwa nyara au kunaswa na wasafirishaji watu kwa njia ya haramu.

Jamaa ya msichana huyo alisema msichana wao alipotea mjini Nairobi tangu Jumamosi baada ya kushawishiwa na waliokuwa wamemuahidi kazi ya maonesho ya urembo.

“Binamu yangu pamoja na wasichana wengine, 16, wakiwa kundi la watu sita, wamepotea tangu wakati huo,” mwanamke huyo amesema kwenye ujumbe alioutuma kwa njia ya video.

Ijumaa, polisi iliandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter kuwa maafisa wa idara ya upelelezi na ulinzi wa watoto wamenusuru wasichana watatu kati ya saba walioripotiwa kupotea. Juhudi za kutafuta wasichana wengine zinaendelea, ilimesema.

Idara hiyo ya upepelezi haikutoa taarifa zozote kuhusu walikokuwa wasichana hao au kama kuna yeyote aliyekamatwa.

Ofisi ya DCI imesema genge hilo linaendesha shughuli zake mjini Nairobi na linatumia nambari ya simu ya kimataifa iliyosajiliwa.

“Wakati uchunguzi unaendelea, tungependa kutoa onyo kwa watu wanaotumia ugonjwa wa Covid-19 vibaya na kuwinda wasichana wa shule, Siku zao zimeisha,” ofisi ya DCI imesema kwenye mtandao wa Twitter.

Mapema mwezi huu, Kenya iliyo Afrika Mashariki, iliongeza masharti ya kukabiliana na virusi vya corona kwasababu ya kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ya ugonjwa huo na vifo.

Mkusanyiko wa watu umepigwa marufuku na amri za kutotoka nje usiku imewekwa. Shule zilifungwa mnamo mwezi Machi mwaka huu lakini mwezi Oktoba zikafunguliwa kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho pekee huku serikali ikitangaza kuwa shule zitafunguliwa tena kikamilifu Januari mwakani.

Kenya yenye idadi ya watu milioni 53, hadi kufikia sasa imetangaza maambukizi zaidi ya 75,000 na vifo 1,349, kulingana na idadi jumla ya Chuo Kikuu cha John Hopkins.

Maelezo ya video,

Virusi vya corono: ‘Wazazi hawana uwezo wa kuniwezesha kudurusu mtandaoni’Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *