Macron: Ulaya itaendeleza mapambano ya ugaidi eneo la Sahel


Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikutana Jumanne na viongozi wa kundi la nchi za Sahel ambazo ni Mauritania, Burkina Faso, Chad, Mali na Niger. Mara baada ya mkutano huo uliolenga kutathmini mkakati mpya katika mapambano na makundi ya kigaidi, Rais Macron alisema kumekuwa na matokeo ya kushangaza kama vile kuyachukua maeneo kutoka mikononi mwa makundi ya kigaidi.

“Muungano tulioutangaza huko Pau miezi sita iliyopita, uko tayari. Ulaya, taasisi zake na nchi wanachama, nchi jirani zote ziko tayari. Na ziko upande wenu kwasababu tunaamini ushindi unawezekana Sahel na hiyo ni sababu inayoamua utulivu wa Afrika na Ulaya,” alisema rais Macron.

Mkutano huo uliitishwa ili kuimarisha mbinu za kimkakati, zilizochochewa na mfululizo wa mashambulizi ya mwaka jana yaliyosababisha askari 13 wa Ufaransa kuuawa katika ajali ya helkopita. Chini ya mabadiliko hayo, Ufaransa iliongeza idadi ya askari 500 katika kikosi chake cha Barkhane cha kupambana na ugaidi ukanda wa Sahel, na kufanya jumla ya askari wake kufikia 5,100. Tangu wakati huo wanajihadi wameendeleza mashambulizi ya karibu kila siku, lakini pia walimpoteza kiongozi muhimu kwenye uvamizi wa vikosi vya Ufaransa na pia mapigano ya ndani.

Niger Niamey | G5-Sahelgipfel | Keïta & Issoufou &Kaboré & Déby & Ghazouani (Getty Images/AFP/B. Hama)

Marais wa nchi za kundi la Sahel

Kinyume na rais Macron, mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Mauritania Ould Ghazouni aliashiria hali ya tahadhari zaidi akisema kumekuwepo na “maendeleo muhimu” lakini hilo “halitoshi katikati mwa ongezeko la changamoto zilizopo”. Pia amesema mgogoro wa Libya ni chanzo kikubwa cha kudhoofika kwa hali ya usalama katika ukanda wa Sahel. Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alihudhuria mkutano huo wakati Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte na rais wa baraza la Ulaya Charles Michel wakishiriki kwa njia ya vidio.

Uasi kaskazini mwa Mali ulianza mwaka 2012 wakati wa uasi wa kundi la wanaotaka kujitenga wa Tuareg ambao baadae lilikuja kudhibitiwa na wanajihadi. Licha ya kuwepo na vikosi vya Umoja wa Mataifa na Ufaransa, mzozo huo umeenea hadi katikati mwa Mali, nchi jirani ya Burkina Faso na Niger. Maelfu ya askari na raia wameuawa na maelfu wengine kuyakimbia makaazi yao. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura Jumatatu wiki hii ya kuongeza mamlaka ya kikosi cha kulinda amani cha MINUSMA nchini Mali kwa mwaka mmoja.

Vyanzo: AFP/DPA

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *