Maduro amtimua balozi wa Umoja wa Ulaya Venezuela


“Tumechoshwa na ukoloni wa Ulaya dhidi ya Venezuela. Balozi wa Umoja wa Ulaya Isabel Brilhante Pedrosa, ana muda wa saa 72 kuondoka Venezuela. Tumechoka na utawala wa wazungu pamoja na ubaguzi,” alisema Rais Maduro katika kasri la Miraflores ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa kutoka serikalini.

Maduro ameongeza kuwa muda umefika muda wa kuweka mipaka ya uhusiano na Umoja wa Ulaya akiongeza kuwa kama wamechoshwa na Venezuela basi waondoke.

Kwa upande wake Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja huo Josep Borrell, amelaani uamuzi wa kumfukuza Balozi Pedrosa. Borrell ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba watachukua mikakati zaidi ya kujibu hatua hiyo ya Venezuela.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliwaweka maafisa 11 wa Venezuela katika orodha ya watu wanaopaswa kuwekewa vikwazo kwa madai ya kuhatarisha demokrasia na utawala wa sheria katika taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Viongozi waliowekewa vikwazo wapigwa marufuku kusafiri Ulaya

Isabel Brilhante Pedrosa (Imago Images/Agencia EFE/M. Gutierrez)

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Venezuela Isabel Brilhante Pedrosa

Maafisa hao wanakabiliwa na marufuku ya kusafiri Ulaya na mali zao kuzuiliwa. Katika taarifa ya Umoja wa Ulaya maafisa hao kumi na moja wanadaiwa kujihusisha pia na kuwaondolea kinga ya bunge wanachama kadhaa wa bunge la nchi hiyo akiwemo kiongozi mkuu wa upinzani, Juan Guaido.

Umoja wa Ulaya unamtambua Guaido kama kiongozi wa bunge la taifa, licha ya uamuzi wa mahakama kuu ya Venezuela mapema mwezi huu, kumuidhinisha mshirika wa serikali Luis Parra kuchukua nafasi hiyo.

Luis Parra ni miongoni mwa maafisa waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya unaouona uteuzi wake kuwa si halali.

Venezuela iliingia katika mgogoro mkubwa wa kung’ang’ania madaraka baina ya Rais Nicolas Maduro na kiongozi wa upinzani, Juan Guaido anayeungwa mkono na Marekani pamoja na mataifa mengi ya Amerika ya Kati na Umoja wa Ulaya. Takriban mataifa 50 ikiwemo Marekani na wanachama wengi wa Umoja wa Ulaya wanamtambua Guaido kama rais wa mpito.

Maduro kwa upande wake anaungwa mkono na China, Urusi na washirika wake wa kimaeneo kama Cuba, Bolivia na Nicaragua.

Vyanzo: dpa/afp

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *