

Maafisa wa polisi wakiwafyatulia risasi waandamanaji Myanmar
Polisi wamepiga risasi na kuwaua waandamanaji 18 nchini Myanmar, ofisi ya Umoja wa Kimataifa ya kutetea haki imesema katika siku ambayo maandamano ya kupinga mapinduzi yamekumbwa na mauaji mabaya.
Vifo vimeripotiwa katika miji kadhaa ikiwemo Yangon, Dawei na Mandalay baada ya polisi kutumia risasi halisi na vitoa machozi.
Vikosi vya usalama vilianza msako uliokumbwa na vurugu siku ya Jumamosi baada ya wiki kadhaa za maandamano ya amani kupinga mapinduzi ya kijeshi ya Februari mosi.
Viongozi wa serikali, miongoni mwao Aung San Suu Kyi, waliondolewa madarakani na kuzuiliwa.
Kanda za video katika mitandao ya kijamii zinaangazia matukio ya siku ya Jumapili zikiwaonesha waandamanaji wakitoroka huku polisi wakiwakimbiza, vizuizi vya muda vya barabarani vikiwekwa, na watu kadhaa waliokuwa wamelowa damu wakielekezwa kwingine.
Oparesheni hiyo iliimarishwa siku ya Jumapili huku viongozi wa mapinduzi wakipambana kuvunja uasi wa raia ambao haujaonesha dalili ya kumalizika.
Mshauri wa Usalama wa Umoja wa Mataifa Jake Sullivan amesema utawala wa Biden unaandaa “hatua za ziada” dhidi ya wale waliyohusika na msako huo wa vurugu.
“Tutaendelea kushirikiana kwa karibu na washirika wetu kuratibu yanayoendelea katika eneo la the Indo-Pacific na ulimwengu mzima kuwawajibisha wanaohusika na vurugu,” alisema katika taarifa siku ya Jumapili.
Marekani tayari imewawekea vikwazo viongozi wa kijeshi wa Myanmar tangu jeshi lilipochukuwa madaraka.
Watu hawakurudi nyuma
Katika eneo la tukio: Mwandishi na mnasa video wa BBC
”Nilipofika katika Barbara ya Hledan mjini Yangon ambulensi ilinipita. Nilisikia mtu mmoja alikuwa amepigwa risasi. Nilikimbilia mahali palipotokea kisa hicho lakini nilipofika wahudumu wa kujitolea walikuwa tayari wamemuingiza kwenye ambyulensi.
Niliona damu barabarani na ngao ya kujitengezea nyumbani kando yake. Risasi ilikuwa imepenyeza kupia ngao hiyo.
Chanzo cha picha, BBC Burmese
Mtu aliyejeruhiwa akipatiwa matibabu katika ambyulensi katika mji wa Hledan huko Yangon
Dakika chache baadae, waandamanaji zaidi waliingia barabarani, kuziba eneo hilo kwa kutumia ngao na mikokoteni wakijiandaa kukabiliana na polisi.
Wengine Wengi zaidi waliwasili, kukaa barabarani wakiimba. Walikuwa wengi sana sikuweza kuona mwisho wa mkusanyiko wa watu.
Watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na mwingine mmoja kujeruhiwa katika eneo hili. Lakini watu hawakurudi nyuma.
Nini kilichofanyika baadae?
Ofisi ya Kutetea Haki ya Umoja wa Mataifa ililaani vurugu dhidi ya waandamanaji, ikisema “taarifa za kuaminika” kwamba watu 18 waliuawa siku ya Jumapili. Wengine zaidi ya 30 walijeruhiwa.
“Watu wa Myanmar wana haki ya kuandamana kwa amani kushinikza kuregeshwa kwa kidemokrasia ,” msemaji Ravin Shamdasani alisema. “Utumizi wa nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hairuhusiwi chini ya maadili ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu.”
Wanaharakati na wahudumu wa afya wamesema karibu watu wanne wameuawa katika mji mkuu, Yangon, baada ya polisi kufyatua risasi, kurusha guruneti ya mkono na vitoa machozi.
Waandamanaji walikataa kuondoka. “Wakitusukuma, tutasimama. Wakitushambulia, tutajilinda. Hatuwezi kupigia magoti ,” Nyan Win Shein aliambia shirika la habari la Reuters.
Mwandamanaji mwingine, Amy Kyaw, aliambia shirika la habari la AFP: “Police walianza kupiga risasi tulipoanza kuwasili. Hawakutoa onyo lolote. Baadhi ya watu walijeruhiwa na baadhi ya waalimu bada wamejificha katika nyumba za majirani.”
Baadhi ya waandamanaji waliingizwa ndani ya magari ya polisi na kuondolewa.
Katika mji wa kusini wa Dawei, vikosi vya usalama viliingilia kati na kuvunja mikutano. Kuna ripoti kwamba risasi halisi zilitumika. Watu wanne waliuawa katika mji huo, wanaharakati waliambia BBC.
Chanzo cha picha, EPA
Waandamanji katika eneo la Mandalay wanataka kuachilia kwa Aung San Suu kyi
Polisi pia walivamia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Mandalay, ambako walitumia maji ya mwasho na kupiga risasi hewani kuwatawanya watu. BBC imefahamishwa kwamba mtu mmoja aliuawa.
Maandamano yalishuhudiwa kwengine, ikiwa ni pamoja na katika mji wa kaskazini mashariki wa Lashio.
Umoja wa Mataifa umesema vifo vimeripotiwa katika miji ya Myeik, Bago na Pokokku.
Idadi ya waliokamatwa tangu maandamano yalipoanza haijabainishwa.
Chama kinachoangazia wafungwa wa kisiasa kinakadiria waliokamatwa ni watu 850, lakini mamia huenda wamezuiliwa wikendi hii.
Waandamanaji walifanya mikutano ya hadhara katika maeneo tofauti barani Asia, ikiwemo Taipei na Hong Kong, kuunga mkono waandamanaji nchini Myanmar.
Huko Bangkok, polisi walitumia vitoa machozi na maji ya mwasho dhidi ya waandamanaji ambao pia walikuwa wakishinikiza kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Thailand.
Aung San Suu Kyi yuko wapi?
Kiongozi huyo wa kiraia wa Myanmar hajaonekana hadharani tangu alipozuiliwa katika mji mkuu wa Nay Pyi Taw mapinduzi yalipoanza.
Wafuasi wake na wegine Wendi katika jamii ya kimataifa wanataka aachiwe huru na kutambuliwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Novemba ambao chama chake cha National League for Democracy kilipata ushindi wa kishindo.
Bi. Suu Kyi anatarajiwa kufika mahakamani Jumatatu kuendelea na mashtaka ya kuwa na kifaa cha mawasiliano ambacho hakijasajiliwa na kukiuka kanunu za kudhibiti virusi vya corona. Lakini mawakili wake wamesema hawajafanikiwa kuzungumza naye.
Viongozi wa kijeshi walichukua madaraka kwa kisingizio kwamba uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu, madai ambayo yamepingwa na kamatii ya uchaguzi.
Mapinduzi yamelaaniwa vikali nje ya Myanmar, hatua iliyochangia vikwazo kuwekwa dhidi ya majeshi na hatua zingine za adhabu.
Maelezo zaidi kuhusu Myanmar
•Myanmar, inajulikana pia kama Burma, ilikuwa chini ya utawala wa kijeshi kuanzia mwaka 1962 mpaka 2011
•Harakati za ukombozi zilianza mwaka 2010, na kulifanya taifa hilo kuwa na uchaguzi huru mwaka 2015 na mwaka uliofuata serikali ya taifa hilo kuanza kuongozwa na kiongozi nguli wa upinzani Aung San Suu Kyi.
•Mwaka 2017, mgogoro mkubwa uliibuliwa na jeshi la Myanmar katika eneo la waislamu wa Rohingya ambapo mamilioni ya watu walikimbilia mpakani mwa Bangladesh, jambo ambalo baadaye Umoja wa Mataifa UN iliita kuwa “mfano wa kitabu cha utakaso wa ukabila”
•Aung San Suu Kyi na serikali yake ilipinduliwa na jeshi Februari 1 February kufuatia matokeo ya uchaguzi wa Novemba.