Marekani yapoteza nusu milioni kwa COVID-19, Ujerumani yasambaza chanjo


Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, idadi ya waliokufa kutokana na corona nchini Marekani sasa imeshapindukia 500,000, ikimaanisha kuwa taifa hilo kubwa kiuchumi ndilo pia kubwa kwenye vifo vya COVID-19, kwani linabeba asilimia 20 ya hivyo pekee. 

Duniani kote, watu waliokwishapoteza maisha kwa virusi hivyo, imekaribia milioni mbini na nusu.

Idadi hii ya Wamarekani waliopoteza maisha kwa corona inapindukia wale waliokufa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vya Vietnam, wakichanganywa pamoja. 

Hapo jana, Rais Joe Biden aliamuru bendera nchi nzima kupepea nusu mlingoti kwa heshima ya wahanga hawa wa COVID-19 na taifa zima kukaa kimya kwa dakika moja kukumbuka mateso waliyopitia raia wenzao wakiwa dakika zao za mwisho za kuaga dunia.

“Kama taifa, hatuwezi kukubali jaala hii ya kikatili. Wakati ambapo tumeshapambana na janga hili kwa muda mrefu, tunapaswa kujizuwia kutokudumazwa na huzuni. Tunapaswa kujizuwia kuyaangalia maisha kama takwimu tu au maruweruwe au taarifa ya habari tu. Tunapaswa kufanya hivyo ili kuwapa heshima maiti wetu, lakini pia kwa umuhimu huo huo iwe ni kuwahudumia waliopo hai bado, wale walioachwa nyuma,” alisema Biden.

Urusi yapoteza watu 400 kwa siku moja

Wakati Marekani ikiomboleza vifo vya watu 500,071 kufikia jioni ya jana, Urusi inasema kufikia sasa imeshapoteza watu 84,047.

Hii ni baada ya hapo kutangaza vifo 417 ndani ya kipindi cha masaa 24 iliyopita.

Hadi sasa, Urusi imesajili watu 4,189,153 waliokwishaambukizwa COVID-19 tangu janga hilo lianze.

Ujerumani yasambaza chanjo

Hapa nchini Ujerumani, kampeni ya kutowa chanjo kwa raia imepamba moto ingawa inakosolewa kwa kwenda kwa kasi ndogo kutokana na upungufu wa vifaa na pia upinzani kutoka kwa baadhi ya watu ambao wanaishuku chanjo itolewayo na kampuni ya AstraZeneca Plc.

Skuli za msingi, kati na maandalizi zilifunguliwa hapo jana, huku mawaziri wa afya wa serikali kuu na serikali za majimbo wakitangaza kwamba sasa walimu watakuwa watu wa mwanzo kupatiwa chanjo kutokana na majukumu waliyonayo.

Waziri wa Afya Jens Spahn ameomba pia chanjo hiyo itolewe kwa maafisa wa polisi na jeshi, baada ya wafanyakazi wa huduma za afya na uokozi kuchanjwa.

Katika mataifa kadhaa ya Ulaya, ikiwemo hapa Ujerumani, chanjo ya AstraZeneca imekumbana na upinzani baada ya kuonesha kuwa haina ufanisi mkubwa inapolinganishwa na chanjo nyengine za Pfizer na Moderna.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *