Marekani yarejesha msaada wa kifedha kwa Palestina


Katika kile kinachoonekana kuwa ni kujetenga kabisa na sera za Donald Trump zilizoipendelea Israel, Biden ametangaza kuwa Marekani itarejesha msaada wake kwa shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Palestina ambalo mtangulizi wake alisitisha kulipatia fedha.

Wizara ya Mambo ya kigeni ya Marekani imesema nchi hiyo itachangia dola milioni 150 kwenye shirika hilo pamoja na kutoa msaada mwingine wa dola milioni 75 kusaidia uchumi na maendeleo kwenye eneo la ukingo wa magharibi na ukanda wa Gaza.

Na hapo jana kwenye mazungumzo ya simu na mfalme Abdullah wa Jordan, taifa ambalo ni mshirika wa muda mrefu wa Marekani, rais Joe Biden alirejea msimamo wake kuwa Marekani inaunga mkono pendekezo la kuundwa mataifa mawili kama njia ya kumaliza mzozo kati ya Israeli na Palestina.

Uamuzi huo ni kwa maslahi ya Marekani 

Palästina UNWRA Symbolbild

Shirika la UNRWA hutoa msaada kwa wakimbizi wa Palestina

Ama kuhusu msaada wa fedha kwa Palestina, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken  amesema kuwa uamuzi huo wa Marekani umezingatia maslahi na maadili ya taifa hilo katika kuwasaidia wenye uhitaji ndani ya Palestina.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu uamuzi huo wa rais Biden msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Ned Price amesema;

“Kwa kurejesha msaada huu leo, siyo kwamba tunakuwa washiriki wa majadiliano pekee bali ni sehemu ya wafanya maamuzi. Tutaweza kuliendesha shirika la UNRWA kwa njia tunazodhani ni kwa maslahi na maadili yetu. Bila shaka kuna maeneo tungehitaji kuona mageuzi. Tutaendelea kuchukua nafasi kubwa zaidi na kulielekeza shirika la UNRWA katika mwelekeo tunaodhani ni wa manufaa”

Hata hivyo kama ilivyotarajiwa Israel ambayo imechukua msimamo wa kuukosoa utawala wa  Biden imesema kurejeshwa msaada  kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa huduma ya maakazi, elimu na usaidizi mwingine kwa zaidi ya wakimbizi wa kipalestina milioni 6 ni jambo la fedheha.

Balozi wa Israel nchini Marekani Gilad Erdan amesema nchi yake inaaminishirika hilo la Umoja wa Mataifa halikupaswa kuwepo wala kupewa fedha.

Palestina yapokea uamuzi huo kwa matumaini 

Kwa Palestina, uamuzi huo wa Marekani umepokewa kwa bashasha na matumaini makubwa na maafisa wake wamesema kuwa hiyo ni hatua ya mwanzo ya utawala wa Biden kuishinikiza Israel ikiwa ni pamoja na baadae kuitaka isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi kwenye eneo la ukingo wa magahribi inalolikalia kwa mabavu.

Waziri mkuu wa serikali ya mamlaka ya ndani ya Palestina Mohammed Shtayyeh amesema wanasubiri kwa hamu siyo tu kurejea kwa msaada wa kifedha bali pia uhusiano wa kisiasa na Marekani ili kuwawezesha watu wa Palestina kupata haki ya kuwa na taifa huru na Jerusalem kuwa mji wake mkuu.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *