Mvua kuendelea kuipiga Kenya


Kitengo cha kupambana na majanga ya kitaifa kinaeleza kuwa watu wasiopungua 130 wamefariki baada ya kuzama kwenye mafuriko au kusombwa na maporomoko ya tope.

Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya,mafuriko yanayoshuhudiwa yataendelea kwa muda wa wiki tatu zijazo hadi wakati wa Krimasi. Hilo huenda likasababisha maporomoko ya tope nyingi zaidi na kuwaacha wengi bila makaazi.

Kulingana na naibu mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya hewa David Gikungu mafuriko na maporomoko ya tope yataendelea kushuhudiwa hasa katika maeneo yaliyo na kinamasi au ya maeneo ya chini. Tayari hali hiyo imeshaanza kuonekana. Katika kaunti ya Makueni watu kadhaa wameachwa bila makaazi baada ya mito kuvunja kingo zake. Kamishna wa kaunti hiyo ya Makueni Mohammed Maalim ameweka bayana kuwa mpaka sasa watu 10 wameripotiwa kufariki.

Kenia Überschwemmungen (picture-alliance/AP)

Abiria akiwa wamekwama kwenye barabara inayotokea Kapenguria, kaunti ya Pokot Magharibi baada ya mvua kubwa kuharibu barabara hiyo.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa imetoa tathmini mpya ya mvua ambayo ilitarajiwa kuacha kunyesha katika wiki ya pili ya mwezi wa Disemba. Mvua hiyo inasababishwa na ongezeko la viwango vya joto kwenye bahari ya Hindi katika maeneo ya Afrika Mashariki linalochangia mvuke mwingi.

Maeneo ya kanda ya ziwa viktoria na milima ya bonde la ufa huenda yakapondwa na dhoruba kali. Kwenye maeneo ya katikati ya Kenya ambayo ni Nairobi, Embu, Nyeri, Meru na yale ya karibu mvua itaongezeka mwezi huu inaeleza taarifa ya idara ya utabiri wa hali ya hewa.

Hapa jijini Nairobi maji yametuama mitaani na barabarani kufuatia mvua hiyo ya kupita kiasi.Kituo cha Mombasa cha utabiri wa hali ya hewa kilirekodi mvua iliyopita asilimia 289 ya kiwango cha kawaida cha mwezi huu.Gavana wa kaunti ya Taita Taveta Granton Samboja amepiga marufuku shughuli za kuchimba mchanga ili kuepusha dharura kufuatia mafuriko eneo hilo.

Maeneo mengine ya pwani nayo pia yamepokea mvua nyingi.Mvua nyingi zaidi imeshuhudiwa kwenye kituo cha Karurumo kilichoko Embu ikifuatiwa na Meru.Takwimu za shirika la msalaba mwekundu zinaashiria kuwa watu wasiopungua 160,000 wameachwa bila makazi tangu mvua kuanza mwezi wa Oktoba.

Yote hayo yakiendelea kitengo cha ndege cha idara ya polisi kimekuwa kikiwanusuru wakazi wanaotatizwa na mafuriko kwa kuwanyanyua kwa helikopta kote nchini.Helikopta 5 kati ya zake zote 7 zinatumika kwenye shughuli za uokozi. TM,DW Nairobi.

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *