Mwanamke ashitakiwa kuchangisha pesa akidai kuwa anaugua saratani


Elkabbass arriving at court

Maelezo ya picha,

Nicole Elkabbas alidai kuwa ana saratani ya kifuko cha mayai ya uzazi

Nicole Elkabbas, 42, alianzisha mchango kwa njia ya mtandao akidai kuwa anahitaji pesa za kugharamia matibabu ya saratani ya kifuko cha mayai ya uzazi katika hospitali moja ya kibinafsi.

Hata hivyo, polisi ilianza uchunguzi baada ya daktari ambaye siku za hivi karibuni alimpima na kumuarifu kuwa yu bukheri wa afya, kuwa na wasiwasi juu ya mienendo yake.

Elkabbas, amekanusha mashitaka hayo na kuambia mahakama kuwa aliamini anaugua saratani.

Jaji Mark Weekes alisema Elkabbas ameshitakiwa kutokana na ushahidi uliotolewa ambao uko wazi na kwamba atarajie kuhukumiwa kifungo kwa kuzingatia sheria.

Maelezo ya picha,

Katika kampeni yake aliweka picha iliyoonesha picha ya wakati wa nyuma akiwa anapata matibabu ya kibofu cha mkojo

Ben Irwin, mwendesha mashitaka, awali alielezea mahakama kuwa hatua za Bi. Elkabbas zilikuwa za kukusudia na “uongo mtupa”.

Februari 2017, mshitakiwa alianzisha kampeni ya kuchangisha pesa kupitia tovuti ya ‘GoFundMe’ ambako alisema ana wiki kadhaa tu za kuchangisha pesa ili akafanyiwe upasuaji nchini Uhispania.

Mwanamke huyo alidai kuwa kuna “dawa” ambayo gharama yake ni ya juu inayotarajiwa kuimarisha hali yake kiafya na pia aliweka picha mtandaoni inayomuonesha akiwa amelala kwenye kitanda hospitalini.

Picha ya uongo

Hata hivyo, mahakama ilibaini kwamba picha hiyo ilichukuliwa wakati wa matibabu ya kawaida ya kibofu cha mkojo miezi kadhaa nyuma.

Bwana Irwin alisema “uongo wa kukusudia” umedhihirika kwenye picha hiyo na kujitokeza wazi kwamba nia yake ilikuwa “kushawishi watu kwamba ni mgonjwa sana”.

Baada ya “kulaghai” watu na kumchangia pesa walizodhani kwamba ni za matibabu, alichofanya ni kuzitumia vibaya pesa hizo kwa kusafiri nje ya nchi, kununua tiketi za kutazama mechi ya mpira wa soka moja kwa moja na kushiriki mchezo wa bahati na sibu mtandaoni, mwendesha mashitaka Bwana Irwin alisema hivyo mahakamani.

Mwanamke huyo atahukumiwa Februari 5 kwa kosa la udanganyifu, kwasababu alijiweka katika hali ambayo haikuwa ya kweli pamoja na umiliki wa mali kwa njia ya uhalifu.

Tovuti ya GoFundMe ilisema kuwa pesa zote zilizochangishwa kwa ajili ya Bi. Elkabbas kupitia mtandao wao zilirejeshwa mwaka jana baada ya kuibuka kwa madai ya utumiaji mbaya wa pesa hizo.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *