‘Nilimkumbatia mwanaume aliyemuua baba yangu’


Candice Mama

Candice Mama alipokuwa na miaka 9, alifungua kisiri ukurasa kwenye kitabu ambacho hakustahili kukiangalia. Picha aliyoiona ilimpa ufumbuzi wa kitu kibaya sana kilichotokea – mwili wa marehemu baba yake aliyekuwa ameuawa. Lakini miaka kadhaa baadae, Candice alikutana na muuaji wa baba yake na kumsamehe – mwanaume aliyefahamika kama “Prime Evil”, Eugene de Kock.

Glenack Masilo Mama aliaga dunia Candice alipokuwa na miezi minane pekee, kwa hiyo binti yake ameishi akifikiria jinsi baba yake alivyokuwa kwa kutilia maanani anayoyasikia kumhusu.

Candice alizaliwa Afrika Kusini mwaka 1991, wakati mfumo wa ubaguzi wa rangi ulikuwa unaanza kuangamizwa taratibu.

Maelezo ya picha,

Candice akiwa mtoto amebebwa na baba yake na aliye kando ni mama yake

Candice alifahamu ziku zote kwamba baba yake aliuawa. Pia alifahamu aliyemuua baba yake – Eugene de Kock, komanda wa kikosi cha polisi cha Vlakplaas, kikosi kilichohusika na kutesa na kuua wanaharakati weusi waliopinga ubaguzi wa rangi. Lakini mama yake hakuwahi kumuarifu hilo.

Alipokuwa na umri wa miaka 9 Candice aligundua taarifa hizo baada ya kubaini kwamba kitabu fulani kinavutia sana wageni wanaomtembelea mama yake.

“Kila wakati wageni wangetutembelea, mama angeliniomba niende kumchukulia kitabu hicho kisha baada ya hapo watu wangelia huku wengine wakipaza sauti zao na kupiga mayowe,” Candice anasema.

“Ningeona mambo ya ajabu ajabu kwa wakati huo niliyachukulia hivyo kisha nikajiambia, najua baba yangu yuko kwenye kitabu hichi, lakini kwanini kila wakati anasababisha kilio kwa wengine?'”

Siku moja akasikia wakizungumzia ukurasa wanaotaka kuutazama.

“Kwahiyo nikajiambia, nikipata nafasi peke yangu pia mimi nitafungua ukurasa huo niutazame.'”

Wiki moja baadae, mama yake alipokuwa ameenda kufanya manunuzi, Candice alipanda juu ya kiti na kufikia kitabu kile kilichokuwa kimewekwa kwenye chumba cha kulala cha mama yake.

Alifungua ukurasa ule aliokuwa ameukariri na kuona picha mbaya mno iliyoonesha mwili wa baba yake uliochomwa moto akiwa ameshika usukani wa gari yeye akiwa dereva.

“Akilini mwangu, moja kwa moja nikaanza kufikiria vile alivyokufa na [Eugene de Kock] ndiye aliyemuua. Nilikikumbatia kitabu kile.”

Maelezo ya picha,

Eugene de Kock alipewa jina la utani la “Prime Evil”

Bila kusema chochote kwa mama yake, Candice anasema hasira aliyokuwa nayo moyoni mwake ilianza kuongezeka na kukua. Na pia hamu yakutaka kujua mengi kumhusu baba yake ikaongezeka.

“Nikaona albamu yake ya picha,” Candice anasema. “Nikaona alichokuwa anakiandika na kubandika kwenye picha zake. Alionekana mwenye kufahamu mengi kuhusu kilichokuwa kinaendelea.

“Kitu kimoja alichosema ni kwamba, kwasababu tu wewe ni mweusi, hakumaanishi kwamba huwezi kufanikiwa.”

Maelezo ya picha,

Baba yake Candice, Glenack Masilo Mama wakati huo akiwa na umri wa miaka 21

Lakini hasira na machungu aliyokuwa anapitia Candice ilifika wakati kukaanza kumuathiri afya yake.

Siku moja akiwa na umri wa miaka 16, alikimbizwa hospitali baada ya kuonesha dalili za mshtuko wa moyo.

“Siku iliyofuata daktari alinikalisha mimi pamoja na mama yangu na kuniambia, unajua kwamba huna mshtuko wa moyo, lakini katika tajriba yangu yote zaidi ya miaka 20 sasa kwenye kazi hii, sijawahi kukutana na mtu mwenye dalili za msongo wa mawazo kama wewe tena kwa umri huu ulionao,'” Candice anasema.

“Sijui ni seme nini lakini hizi dalili zote unamaliza mwili wako na ikiwa hutabadilika utafariki dunia.'”

Huo ndio ulikuwa mwazo wa Candice kubadilika.

Mwaka 1995, baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia, serikali ya Afrika Kusini iliyokuwa inaongozwa na Nelson Mandela, iliunda Tume ya Ukweli na Maridhiano kusikiliza ushahidi wa waliokiuka haki za binadamu chini ya utawala wa Ubaguzi wa rangi.

Nyaraka zote zikawekwa mtandaoni na Candice alipata fursa ya kusoma kwa makini kuhusu aliyemuua baba yake Eugene de Kock.

Lakini baada ya muda, alifikia kile ambacho wengi hawakudhania, kumsamehe mwanaume aliyemuua baba yake.

“Ilianza kama kutaka kulipiza kisasi, kwasababu nilijifikiria mimi tu, Kila wakati ninapomfikiria mwanaume huyu huwa ni kama ananidhibiti, Nashtuka. Ni kama siwezi kudhibiti hisia zangu.’ Nilikuwa nikifikiria amemuua baba yangu na sasa ataniua mimi.’ Kwa hiyo kwangu msamaha ilikuwa jambo la msingi sana.”

Candice alianza kuhisi ameanza kuwa huru.

Mwaka 2014, mama yake Candice alipigiwa simu kuulizwa na mamlaka ya mwendesha mashtaka kama yeye na familia yake ingependa kushiriki kwenye majadiliano ya maridhiano pamoja na kukutana ana kwa ana na Eugene de Kock.

Na moja kwa moja Candice alimjibu mama yake na kusema kuwa yeye binafsi anataka sana kukutana na tume hiyo.

Maelezo ya picha,

Glenack akiwa na kiongozi wa PAC Zeph Mothopeng, ambaye Candice anasema alikuwa kama mshauri wake

TBaada ya kuwasili kwenye chumba cha maridhiano, familia ilianza kuzungumza na walinzi wa wafungwa, washauri na kasisi, lakini ghafla Candice alipotazama tena kwenye chumba hicho, akaonana jicho kwa jicho na Bwana Eugene de Kock.

“Nilipomuona ni kama mwili wangu uliganda kidogo. Kuanzia picha ambazo nimekuwa nikiziona kutoka nikiwa mtoto alikuwa yule yule, sikuamini macho yangu,” Candice anasema.

Mama yake Candice alianza kwa kuuliza kilichotokea siku ile Machi 26, 1992 siku ambayo mume wake alifariki dunia.

Eugene akawaambia kwamba yeye na timu yake walituma majasusi katika kambi aliyokuwa baba yao kubaini wanaharakati waliokuwa na msimamo mkali – na baba yao na wanaume wengine watatu wakabainiwa.

Timu ya Eugene ilichofanya ni kuwafuatilia hadi walipoanza safari yao, walipofika katikati, wakawamiminia risasi na walipowafyatua lakini wanaona ni kama kuna bado wako hai, waliwasha moto gari lao.

Maelezo ya picha,

Candice na familia yake walipoenda kukutana na Eugene de Kock

Wakati huo Candice akasema,

“Eugene nataka kusema nimekusamehe, lakini kabla ya kufanya hivyo, nataka kujua kitu kimoja.’

‘Wewe mwenyewe umejisamehe?’

Kwanza Bwana Eugene alipigwa na butwaa na kusema, “Kila wakati familia inapokuja hapa, hilo ni moja ya swali ambalo huwa naomba wasiliulize.”

“Aliangalia kando na kufuta chozi kwenye jicho moja huku akisema, ‘Wakati umetenda kama yale niliyotenda mimi, unajisamehe namna gani kwa mfano?'”

Candice alianza kulia, sio kwa ajili yake lakini kwasababu ya baba yake – kwasababu alijua kuwa de Kock hatawahi kuwa na amani maishani mwake.

“Tulikuwa watu wawili ambao sote tumeumizwa moyo, tukiwa tunaangaliana, kilikuwa kipindi muhimu sana cha mabadiliko,” Candice anasema.

Maelezo ya picha,

Candice Mama akizungumza katika wakfu wa Nelson Mandela

Na mwisho wa mazungumzo, Candice alisimama na kuelekea alikokuwa ameketi Eugene de Kock na kuuliza ikiwa anaweza akamkumbatia.

“Alipiga magoti na akanikumbatia huku akisema, ‘Samahani kwa kile ambacho nimekutendea, na bila shaka baba yako anafurahia jinsi ambavyo umebadilika na kuwa leo hii.'”

Mwaka 2015, Eugene alipewa msamaha kitu ambacho Candice na familia yake wanakiunga mkono.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *