Ramaphosa azuru Tanzania


Baada ya miezi minne kupita tangu aingie madarakani, Rais Ramaphosa anatua katika ardhi ya Tanzania akitarajia kujadiliana mengi na mwenyeji wake, Rais John Magufuli; ambaye naye pia miezi minne iliyopita alikuwa mjini Pretoria kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Ramaphosa.

Ziara yake hiyo ya siku mbili inatafsiri uhusiano wa miaka mingi kati ya mataifa hayo mawili ulioasisiwa tangu wakati wa harakati za kupigania ukombozi kusini mwa afrika hadi enzi mpya ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya kiuchumi baada ya ukoloni mkongwe.

Afrika Kusini, ambayo pia mwanachama wa mataifa yanayoinukia kwa kasi kiuchumi duniani, BRICS, ni miongoni mwa mataifa machache yenye kiwango kikubwa cha uwekezaji nchini Tanzania.

Kwa hivyo, mbali ya kuwa ziara ya Ramaphosa – mwenye utajiri mkubwa wa binafsi – kuwa mwendelezo wa uhusiano wa kijadi, inatarajiaw kubeba sura ya kiuchumi na masuala ya kibiashara.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa, Innocent Shoo, anasema Afrika Kusini ni taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi Afrika, hivyo “kuna uwezekano mkubwa viongozi hao watapokutana wataafikiana juu ya masuala yenye maslahi kwa pande zote.”

Mbali na hilo, jambo lingine linalotajwa sana na ambalo huenda likapewa nafasi kwenye ziara hii ni kuhusiana na mpango wa Tanzania kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Afrika Kusini.

Kuna ripoti zinasema kwamba Afrika Kusini inakusudia kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa moja ya lugha zitakazopewa umuhimu mkubwa katika shule zake.

Walipokutana mara ya mwisho mwezi Mei nchini Afrika Kusini, wote wawili walidokeza juu ya jambo hilo huku Rais Magufuli akisisitiza azma ya Tanzania kupeleka walimu wake nchini humo.

Masuala ya usafiri wa anga yanatazamiwa vile vile kujitokeza pia kwenye ziara hiyo hasa, wakati huu ambapo Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) likifufuliwa upya na kuanzisha safari zake za moja kwa moja kuelekea Afrika Kusini.

George Njogopa/DW Dar es SalaamSource link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *