Selemani Jafo: Serikali Tanzania yasema walioenguliwa uchaguzi wa mtaa ruhsa kushiriki, ACT chasisitiza hakitoshiriki


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo

Image caption

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo amesema kuwa mamlaka ya uchaguzi imetoa nafasi ya wazi kwa wote bila pingamizi

Serikali Tanzania imewarejesha wapinzani walioenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka wananchi wote waliochukua fomu na kuzirejesha kushiriki kugombea.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo amesema kuwa mamlaka ya uchaguzi imetoa nafasi ya wazi kwa wote bila pingamizi.

“Wale wote walichukua fomu zao na kurejesha fomu zao, nazungumzia wale asilimia 97.3 yani hapa hakuna kukimbiana…”hakuna kuweka mpira kwapani, hapa lazima kieleweke tarehe 24 Novemba”.

Aliongeza kusema kuwa kuna wanachama wa vyama hivyo bado wanapenda kuendelea licha ya viongozi wao kukataa kushiriki.

Wiki iliyopita vyama kadhaa vya upinzani nchini Tanzania vilitangaza kujiondoa katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24.

“Mchakato mzima wa kuchagua wagombea ulifuata utaratibu kwa weledi mkubwa na tatizo lilikuwa ni kwa wagombea na vyama vya siasa kutowapa muongozo mzuri wanachama wao” amefafanua Jafo katika mkutano na waandishi habari.

Waziri huyo anasema kuwa “kulikuwa na makosa mengi ya kikanuni ambapo wengine walijidhamini wenyewe, walitofautiana kwa majina, umri wamekosea….unakuta mtu anaandika amezaliwa 2019.”

“Kama wagombea hao waliteuliwa na vyama vyao na wakafanikiwa kuchukua na kurejesha fomu za kugombea watashiriki kugombea, hakuna kukimbiana” alisema.

Aidha alisema wale ambao hawataruhusiwa ni wale ambao hawana uraia wa Tanzania.

Wapinzani washikilia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi.

Haki miliki ya picha
Getty Images

Wakati huo huo vyama vikuu vya upinzani Chadema na ACT-Wazalendo wameonekana kuendelea na msimamo wao wa kugomea uchaguzi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa Jumatatu kinamwandikia barua Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo kutotumia jina na nembo ya Chadema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu chama hicho kimejitoa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema bwana John Mnyika amesema kwamba chama hicho kimejitoa kwa sababu ya uonevu uliofanyika kwenye mchakato mzima.

“Sisi kama chama tutamwandikia barua waziri Jafo kuwa tumepiga marufuku kutumia jina la Chadema au nembo yake katika mchakato wa uchaguzi kwa sababu tumejitoa,” amesema Mnyika.

Unaweza pia kusoma:

”Takribani, wananchi 173,593. Hata hivyo, kati ya wagombea wetu hao 173,593 waliochukua na kurejesha fomu za uteuzi, 166,649 walienguliwa katika mchakato wa Uchaguzi nchi nzima kwa sababu mbalimbali za kipuuzi na zisizo na mashiko kabisa kama ilivyoelezwa na Viongozi wetu katika nyakati mbalimbali za mchakato huu. Wanachama wa ACT waliobakizwa kwenye Uchaguzi mpaka saa Sita kamili mchana leo ni 6,944 tu sawa na 4% ya wagombea wote tulioweka.” Alisema Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT wazalendo katika mkutano na waandishi wa habari wakati akitangaza chama chake kujiondoa.

Aidha serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya ndani katika Ofisi ya Rais, Tamisemi imesema uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika kama ulivyopangwa tarehe 24 mwezi Novemba mwaka huu.

Ufafanuzi huo umetolewa mapema hii leo katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni, Dodoma ambapo mbunge wa Singida Kaskazini Justice Monko alitaka ufafanuzi wa serikali hasaa baada ya Chama kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Chadema kutangaza kujitoa rasmi katika mchakato wa uchaguzi huo.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *