Sudan yafunga shule baada ya mauaji ya wanafunzi


Siku ya Jumanne mamia ya wanafunzi waliandamana katika mitaa ya mji wa Khartoum, wakiwa wamevalia sare zao za shule huku wakipeperusha bendera za Sudan na kukariri maneno ya “kuuwa mwaanfunzi ni kuuwa taifa.”

Maandamano ya hapa na pale ya wanafunzi yalifanyika pia katika sehemu nyingine za Khartoum na miji mingine.

Wanafunzi watano wa sekondari walipigwa risasi na kuuawa na wengine zaidi ya 60 walijeruhiwa, baadhi na walenga shabaha, walipoandamana mjini Al-Obeid kupinga uhaba wa mafuta na mkate.

Sudan | Streik (Getty Images/AFP/A. Shazly)

Maandamano yameikumba Sudan tangu mwaka uliyopita.

Na Jumanne jioni kamati ya madaktari wanaoegemea vuguvugu la maandamano ilisema mwandamanaji wa sita alifariki dunia baada ya kupigwa risasi kichwani. Lakini kama hiyo haikusema iwapo yeye pia alikuwa mwanafunzi.

Waandamanaji walikituhumu kikosi kinachoogofya cha Rapid Support Forces (RSF) kwa kuwauwa wanafunzi hao.

Amri ya kufungwa kwa shule Sudan

Shirika la habari la serikali ya Sudan (SUNA) limeripoti Jumanne usiku, kuwa baraza la kijeshi limewaagiza magava wa majimbo yote kuzifunga shule za chekechea, msingi na sekondari kuanzia Jumatano hadi itakapotolewa taarifa nyingine.

Mauaji hayo yalitokea siku moja kabla viongozi wa maandamano wafanye mazungumzo na majenerali wa baraza la kijeshi juu ya masuala yaliosalia kuhusu kuundwa kwa serikali ya kiraia baada ya pande mbili kusaini makubaliano ya kugawana madaraka mapema mwezi huu. Lakini viongozi wa maandamano walifuta mkutano uliokuwa ufanyike Jumanne.

Mkuu wa Baraza la kijeshi Adel Fattah al-Burhan alisema katika mahojiano yaliotangazwa Jumanne usiku kuwa mauaji ya wanafunzi hao yalikuwa tukio la kusikitisha na kutoa wito wa kurejea haraka kwenye meza ya mazungumzo kukamilisha mchakato wa mpito wa kisiasa.

Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan (picture-alliance/AA)

Mkuu wa Baraza la Kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesema mauaji ya ya raia hayakubaliki.

“Kilichotokea mjini al-Obeid na kila kitu kilichotokea kabla ni mambo yanayosikitisha. Hakuna anayekubali vifo au mauwaji ya raia yeyote wa Sudan, na hii inaweza kuwa mojawapo ya sababu zinazotusukuma kusaini makubaliano haraka iwezekanavyo kurejesha maisha katika hali ya kawaida.”

Maandamano ya kuipinga serikali yalianza mwishoni mwa mwaka uliopita ambapo waandamanaji walikuwa wakishinikiza kuhitimishwa kwa utawala wa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir. Jeshi liliingilia kati mwezi Aprili, na kumpindua al-Bashir kabla ya kumtia mbaroni.

Lakini waandamanaji wanahoji kuwa watawala wapya wa kijeshi ni mwendelezo wa utawala wa zamani wa Al-Bashir na wametaka muafaka zaidi na kuhamisha madaraka kwa serikali ya kiraia.

vyanzo: mashirika

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *