Tabia duni za watoto wanaoishi gerezani na mama zao wafungwa Kenya


Gereza la lang'ata

Kwa miaka mingi sasa, wafungwa katika magereza ya wanawake nchini Kenya wamekua wanaruhusiwa ndani na watoto wao hadi wanapotimia miaka minne ndio watoto hao wanaachana na mama zao.

Lakini baadhi ya wanaharakati wa kupigania haki za binadamu wanasema si vizuri mtoto kuishi jela na mamake kwani ananyimwa haki yake ya maisha bora.

Wanataka sheria hiyo ibabadilishwa John Nene amezungumza na baadhi ya wahusika na kutuandalia ripoti hii maalum ambayo pia inaangazia kwa undani maisha ya watoto hao gerezani, changamoto za mama wafungwa na watoto wao huko ndani na jinsi maisha hayo ya jela yanaathiri watoto hao kitabia.

Bernard Mbugua hatasahau maisha duni alioyapitia katika jela ya wanawake ya Langata mjini Nairobi akiwa mtoto wa chini ya umri wa miaka minne.

“Yalikua ni maisha ya shida, kuoga ni mara moja kwa wiki na mavazi pia ni tabu kwa watoto wengi hapo ndani,” anasema Mbugua ambaye sasa ana umri wa miaka 18.

Mbugua hakuwa mfungwa katika jela hiyo ya Langata. Alijipata yuko gerezani kwa makosa ya mamake mzazi ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka minne kwa kupatikana na kosa la kuuza pombe haramu.

Sheria ya Kenya kwa hivi sasa inamruhusu mama afungwe na mtoto wake wa chini ya umri wa miaka minne.

Hivyo basi Mbugua akajikuta ni miongoni mwa watoto walioko gerezani lakini si wafungwa.

“Hayo maisha yetu tukiwa huko ni kama wafungwa tu kwa sababu hatuwezi kulala nje. Tena la kuudhi kabisa tunalala chumba kimoja, kitanda kimoja na mama zetu na wafungwa wengine ambao lugha yao chafu, si mfano mzuri kwa watoto wadogo wasio na hatia lakini wanajifunza matusi ya kila aina wanayosikia kwa wafungwa hao.

“Mimi sikubaliani kabisa na sheria hiyo ya watoto kufungwa na mama wao. Iondolewe kwa sababu inamtesa mtoto. Kama huna mtu anakujua utajipata umevaa mavazi hayo hayo mpaka baadae yaanze kunuka.”

Mashirika ya haki za kibinadamu yanapinga vikali sheri hii, na wanataka ing’olewe. Wakfu wa Legal Resources Foundation Trust ni miongoni mwa wanaotaka sheria hiyo ya kuruhusu mama afungwe akiwa na mtoto wake ifutiliwe mbali.

Mratibu wa wakfu huo, Lenson Njagi Njogu anasema:“Tunapinga vikali kuwekwa kwa watoto gerezani, haki yake haijazingatiwa. Watafute njia mbadala. Tushaanza kampeini ya sheria hiyo kupigwa marufuku na wahusika katika serikali ya Kenya.

Hii kwa hakika si sheria nzuri maanake inamnyima mtoto haki yake ya kukuuzwa katika mazingira yafaayo, malezi bora, kwenda shule nzuri na kucheza na wenzake maeneo mazuri.

“Kwa mfano kule Afrika Kusini mama anapopatikana na hatia ya kufungwa jela na ana mtoto, kwanza anapewa nafasi ya kulea mtoto wake kisha akifikisha zaidi ya umri wa miaka mitano anaingia jela sasa kutumikia kifungo chake.”

Swali nyeti hapa ni je, nchini Kenya inawezekana mama apewe nafasi ya kumlea mwanao na hatimaye aingie jela kutumikia kifungo chake?

Baadhi ya Wakenya nchini humo wanasema ni vigumu kwani mfungwa atajaribu kutoroka ahamie taifa lingine ama kaunti nyingine ahepuke kifungu hicho.

Maisha ya gerezani kwa mama wafungwa na watoto wao ni mzigo mkubwa, kama wanavyotueleza wafungwa hawa niliozungumza nao katika jela ya wanawake ya Langata mjini Nairobi.

“Mimi ni mama Saviour, nilikuja hapa Langata mwaka wa 2017 mwezi wa saba. Maisha ya hapa si mazuri ni shida tupu. Pesa za matumizi kwa watoto wetu hatuna, hasa za kununua diapers. Nguo pia ni shida mpaka wageni waje watusaidie. Hapa tunatesa mtoto kwa sababu hana hatia.Ni uchungu sana kufungwa na mtoto wako.”

Mama Kamau ama Jacqueline kwa jina lake naye anapendekeza wapate kifungo cha nje na watoto wao kuhepuka maisha magumu ya jela.

“Mtoto hana makosa hata kidogo sioni kwa nini niwe naye hapa. Lakini pia ni shida abaki nje kwa sababu hakuna mtu wa kumuangalia. Naskia vibaya sana kuwa na mtoto wangu hapa ndani. Maisha yake yote anajua tu askari jela na polisi.”

Kwa hivi sasa jela ya wanawake ya Langata ina jumla ya watoto 32, na ni jukumu la jela hiyo kuwalea watoto hao na mama zao. Jane Kiiri, mkuu wa jela ya wanawake ya Langata, anatueleza miongoni mwa changamoto zinazowakabili wafungwa hao, hali ambayo inachangia kwa watoto hao kutopata malezi bora.

“Hawa kina mama wanapokua hapa jela wana mawazo mengi sana. Wanafikiria watoto wale wamewaacha nje wanakula nini, kwa hivyo inakua vugumu wawape watoto wao wachanga malezi bora.

“Mavazi ni shida kwa sababu hatuna bajeti yake, sasa ndio tutajaribu kuzungumza na serikali watusaidie. Vyakula pia ni shida na wanapougua kuwapa matibabu ni mzigo mkubwa kwetu hapa gerezani. Tunaomba wadhamini wanao jiweza watusaidie kwa hali na mali kwa sababu mzigo huu tunaoubeba ni mzito mno. Wana saikolojia pia tunahitaji huduma zao waje kuzungumza na mama hawa wafungwa.”

Maisha hayo ya gerezani yana athari zake, kama asemavyo Jane Onyango ambaye ni afisa mkuu wa kuangalia maslahi ya wafungwa jela ya Langata.

“Watoto hawa kufungwa na mama ina athari zake wakiwa wakubwa,” anasema Bi Onyango,“Huyo mtoto hataogopa kufanya kosa huko nje afungwe kwa sababu alipokua jela hakuna kazi alifanya ama kuadhibiwa. Kwa hivyo kwake anaona maisha jela ni ya starehe. Kula na kulala.”

Onyango anasema watoto hao wanapotimiza miaka minne kisheria huachiliwa waende kwa vituo vya kusimamia watoto kwa sababu akiwa huo umri ni mtu anajua kabisa mambo yanayoendelea jela.

“Siku ya watoto hao kuondoka huwa ni ya majonzi kwa mama mfungwa kuachana na mtoto wake lakini inabidi,” anasema Onyango.

“Hatahivyo wakiwa katika vituo vya kulea watoto sisi hupanga siku wanaletwa kujiunga na wazazi wao, wale vizuri na wanywe pamoja kisha wanarudishwa huko. Hii ni kuhakikisha hatumnyimi mtoto haki ya kumtembelea mama yake.”

Wengi wa watoto hao hupelekwa kituo cha kulea watoto kiitwacho Nest Childrens Home eneo la Limuru. Ni kama umbali wa kilomita 40 kutoka katikati mwa jiji la Nairobi.

Lucy Nduta ni mmoja wa wahudumu wa kituo hicho cha Nest Childrens Home kilichoanzishwa miaka 27 iliyopita na mkurugenzi mkuu, Irene Baumgartner kutoka Ujerumani.

“Hapa tunalea zaidi ya watoto 70 wa wafungwa katika jela za wanawake sehemu mbali mbali za Kenya,” anaeleza Nduta, “Tuko pia na watoto ambao wamekosa malezi bora huko nje ama wameachwa na wazazi wao. Hawa mama wafungwa wanapoachiliwa wanakuja hapa tunawapa malazi na watoto wao ili waanze kuzoeana baada ya kutengana kwa muda mrefu. Tunawaelimisha, kuwavalisha na kuwasomesha. Huu ni mzigo ambao tunaomba wahisani watusaidie.”

Nduta anatueleza jinsi wao huwa na shida kubwa ya kulea watoto ambao hufungwa na mama zao katika jela za wanawake nchini Kenya.

“Unajua hawa watoto wametoka mahali walikua wanaisha maisha magumu. Sasa tabia zao na lugha ni tofauti kabisa na hawa watoto wengine ambao hawakua jela.

“Lugha yao ni ya matusi na wanapenda vita. Wakiwa kwa mabweni utawajua kwa tabia zao chafu maanake hayo mambo wameyaona yote huko jela. Ukiwapa vitu vya watoto vya kuchezea hawataki mwenzao karibu. Ni wagumu sana kulea na hii inatokana na wao kuishi jela.”

Ndio kwa maana wakfu wa Legal Resources Foundation Trust wanapinga kabisa mtoto kuwa gerezani na mama yake. Kulingana na mratibu wa wakfu huo, Lenson Njagi Njogu, wanakaribia kufaulu kuishawishi serikali iondowe sheria hiyo inayomruhusu mama afungwe jela na mtoto wake aliye chini ya umri wa miaka minne.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *