TikTok: Trump amesema atapiga marufuku programu ya video ya China


President Donald Trump

Maelezo ya picha,

Trump amesema anaweza kupiga marufuku programu hiyo hata kuanzia Jumamosi

Rais Tump ametangaza kwamba anapiga marufuku programu ya video maarufu ya TikTok inayomilikiwa na China nchini Marekani.

Aliwaambia wanahabari kwamba anaweza kutia saini agizo la rais hata Jumamosi.

Maafisa wa usalama Marekani wameonesha wasiwasi kwamba programu hiyo ya kampuni ya ByteDance ya China, inaweza kutumiwa kukusanya data binafsi za raia wa Marekani.

TikTok imekanusha madai kwamba inadhibitiwa na au inashirikisha data zake na serikali ya China.

Programu hiyo ambayo imepata ushawishi kwa haraka ina watumiaji karibu milioni 80 kila mwezi nchini Marekani na marufuku hiyo itakuwa pigo kubwa kwa kampuni ya ByteDance.

“Kampuni ya TikTok, tunaipiga marufuku Marekani,” Bwana Trump amewaambia wanahabari.

Haikubainika mara moja ni mamlaka gani aliyonayo Trump ya kupiga marufuku TikTok, vile marufuku hiyo itakavyotekelezwa na changamoto za kisheria anazoweza kukumbana nazo.

Inasemekana kwamba kampuni ya Microsoft imekuwa ikifanya mazungumzo ya kununua programu hiyo kutoka kwa kampuni ya ByteDance, lakini Bwana Trump ameonekana kutilia mashaka kuwa makubaliano kama hayo yanaweza kufanyika.

Ikiwa makubaliano hayo yataafikiwa, taarifa zinasema kwamba itajumuisha kampuni ya ByteDance kumaliza shughuli zake kupitia programu ya TikTok Marekani.

Msemaji wa programu ya TikTok amekataa kuzungumza lolote dhidi ya hatua ya Trump lakini amearifu vyombo vya habari kwamba kampuni hiyo ina matumaini makubwa ya mafanikio ya muda mrefu Marekani.

Hatua ya kupiga marufuku programu ya TikTok inawadia wakati ambapo kuna wasiwasi kati ya utawala wa Trump na serikali ya China kuhusu masuala kadhaa ikiwemo mzozo wa kibiashara na vile China ilivyoshughulikia mlipuko wa janga la virusi vya corona.

TikTok ni nini?

Programu hiyo imepata umaarufu mkubwa miaka ya hivi karibuni, hasa kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.

Wanatumia programu hiyo kushirikishana video ya sekunde 15 ambayo mara nyingi hujumuisha kuiga nyimbo fulani, wachekeshaji wakifanya vimbwanga vyao na mifumo isiyo ya kawaida ya kubadilisha picha na vyinginevyo.

Video hizo huweza kufikiwa na wafuasi wa programu hiyo na hata wageni. Kimsingi, akaunti zote zinaweza kuonekana na kila mmoja ingawa watumiaji wanaweza kuweka masharti ya video wanazotaka kupakua kwa orodha ya watu kadhaa tu waliowachagua wenyewe.

TikTok pia inaruhusu ujumbe wa kibinafsi kutumwa lakini huduma hii ni kwa marafiki pekee.

Inasemekana kwamba programu hii ina watumiaji karibu milioni 800 kila mwezi wengi wao wakiwa ni kutoka Marekani na India.

India tayari imepiga marufuku programu ya TikTok pamoja na programu zingine za China.

Australia, ambayo tayari imeshapiga marufuku kampuni ya Huawei na ile ya utengenezaji bidhaa za mawasiliano ya ZTE, pia inafikiria kupiga marufuku programu ya TikTok.

Kwanini Marekani inawasiwasi kuhusu programu ya TikTok?

Maafisa Marekani na wanasiasa wameonesha wasiwasi wao kuhusu data inayokusanywa na kampuni ya ByteDance kupitia programu ya TikTok kwamba huenda ikakabidhiwa serikali ya China.

Nchini China, TikTok inatoa huduma sawa na hiyo lakini kupitia toleo jinginge la programu ya China inayofahamika kama Douyin.

Pia inasema data ya watumiaji wote wa Marekani inahifadhiwa Marekani huku chelezo cha programu hiyo ikiwa Singapore.Wiki hii, kampuni ya TikTok iliwaambia watumiaji wake na wadhibiti kwamba huenda ikawa na uwazi wa hali ya juu ikiwemo kuruhusu kupitiwa tena kwa mfumo huo.

“Hatuko kisiasa, haturuhusu matangazo ya kisiasa na hatuna ajenda yoyote – lengo letu kuu ni kuendelea kusisimua, kuwa mtandao ambao kila mmoja ataufurahia,” amesema Mkurugenzi mtendaji wa TikTok, Kevin Mayer, wiki hii.

“TikTok imekuwa mlengwa mkuu, lakini sisi sio adui.”Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *