Ufaransa na nchi za Sahel kutathmini vita dhidi ya makundi ya kigaidi


Viongozi wa nchi za eneo linalokabiliwa na machafuko la Sahel pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakutana mjini Nouakchott, Mauritania ili kuongeza juhudi za kijeshi katika kukabiliana na wanamgambo wa eneo la Sahel.

Mkutano huo unajiri miezi sita baada ya ule uliofanyika Januari 13, katika mji Pau, kusini wa Ufaransa ambao viongozi wa Ufaransa na Afrika Magharibi waliapa kuongeza juhudi za pamoja za kijeshi katika ukanda wa Sahel ambao umelishudia ongezeko la vurugu na umwagikaji wa damu. Mkutano huo uliitishwa baada ya kuuawa kwa wanajeshi 13 wa Ufaransa kwenye operesheni za kijeshi.

Marais wa Mali, Burkina Faso, Chad, Niger na Mauritania wametarajiwa kufanya mazungumzo ya pamoja na Rais Macron kuzungumzia suala la usalama wa eneo la Sahel katika mkutano huo wa kilele. Mbali na operesheni za kijeshi, hakujawa na hatua kubwa katika maridhiano na mageuzi ya kisiasa nchini Mali, ambako ni kitovu cha machafuko hayo ya Sahel.

Mbali na marais hao sita kuna wajumbe pia wa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa, Francophonie, na wale kutoka Umoja wa Ulaya. Kikao hicho kitawashirikisha pia viongozi wa Ujerumani, Uhispania na Italia kwa njia ya video. Hiyo ni ziara ya kwanza ya Rais Macron nje ya Ulaya tangu lilipozuka janga la virusi vya corona.

Mwanajeshi wa kikosi maalumu cha Ufaransa nchini Burkina Faso

Mwanajeshi wa kikosi maalumu cha Ufaransa nchini Burkina Faso

Mnamo kipindi cha miezi sita iliyopita Ufaransa iliongeza idadi ya wanajeshi wake kwenye ukanda wa Sahel na kufikia jumla ya wanajeshi 5,100. Siku za hivi karibuni operesheni za pamoja za wanajeshi wa Ufaransa wa kikosi cha Barkhane na wale wa nchi tano za eneo la Sahel, walizidisha operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa kiislamu kwenye mpaka wa Mali, Burkina Faso na Niger.

Ofisi ya rais wa Ufaransa ilielezea kwamba mkutano huo wa Nouakchott utafungua ”kipindi cha kudumisha” amani kwenye eneo hilo la Sahel. Ufaransa na nchi hizo tano katika eneo la Sahel zilikubaliana kuongeza idadi ya vikosi vya usalama katika mpaka wa Mali, Niger na Burkina Faso ili kuimarisha ulinzi maana wanamgambo wenye silaha wamekuwa wakivuka katika mipaka hiyo kwa urahisi.

Mafanikio makubwa hivi karibuni ni kuuwawa kwa kiongozi wa kundi la Al-Qaida kwenye nchi za Maghreb, Abdelmalek Droukdal mwenye asili ya Algeria, na vikosi maalumu vya Ufaransa vilivyosaidiwa na ndege isiyo na rubani ya Marekani.

Vyanyo: AFPE/AFPF

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *