UNICEF: Covid huenda ikasababisha mamilioni ya ndoa zaidi za utotoni


“Kufungwa kwa shule, msongo wa kiuchumi, kuvurugwa kwa huduma na vifo vya wazazi kutokana na janga la Covid-19 vinawaweka wasichana walio katika mazingira hatarishi zaidi, kwenye hatari inayoongezeka ya kuozeshwa wakiwa watoto,” ulisema utafiti uliopewa jina la “Covid-19: Kitisho kwa mafanikio dhidi ya ndoa za watoto.”

Mwelekeo huo, ikiwa utathibishwa, utasababisha kurejea nyuma zaidi mafanikio ya miaka kadhaa dhidi ya ndoa za watoto. Katika miaka 10 iliyopita, kulingana na utafiti huo, kiwango cha wanawake wadogo walioolewa wakiwa watoto kilipungua kwa asilimia 15, kutoka karibu moja katika wanne hadi moja katika watano.

Mafanikio hayo, “hivi sasa yanakabiliwa na kitisho,” ilisema ripoti ya utafiti huo, iliyotolewa kwenye siku ya Wanawake Duniani. “Covid-19 imeifanya hali ambayo tayari ni ngumu kwa mamilioni ya wasichana kuwa mbaya zaidi,” alisema mkurugenzi mtendaji wa Unicef Henrietta Fore.

“Shule zilizofungwa, kutengwa na marafiki na mitandao ya msaada, na umaskini unaoongezeka vimeongeza mafuta kwenye moto ambao dunia ilikuwa inapambana kuuzima.”

UNICEF | Henrietta H. Fore

Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Henrietta Fore.

Soma pia: Kiongozi wa kimila Malawi aagiza kufutwa kwa ndoa za karantini

Wasichana wanaoolewa utotoni, ulisema utafiti huo, wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupitia vurugu za majumbani na uwezekano mdogo wa kusalia shuleni. Wanakabiliwa na hatari inayoongezeka ya mimba za mapema na zisizo na mpangilio, na matatizo ya uzazi na vifo.

Kutengana na familia na marafiki kunaweza kuwa na “madhara makubwa sana kwenye afya aya akili yao.”

Wakati huo, vikwazo vya usafiri vinavyohusiana na janga la covid-19 na umbali kati ya mtu na mtu vilifanya iwe vigumu zaidi kwa wasichana “kupata huduma za kiafya, huduma za kijamii na msaada wa kijamii unaowalinda dhidi ya ndoa za utotoni, mimba zisizotakiwa na vurugu za kijinsia,” huku vikiongeza uwezekano wa wao kuacha shule.

Zaidi ya hayo, familia zinazokabiliana na hali ngumu kiuchumi zinaweza kutafuta kuwaozesha watoto wao ili kupata ahueni ya mzigo wa kifedha. Ripoti hiyo inakadiria kuwa wasichana milioni 650 na wanawake walio hai leo, waliolewa wakiwa watoto, karibu nusu yao kutoka Bangladesh, Brazil. Ethiopia, India au Nigeria.

Fore alitoa wito kwa mataifa kufungua tena shule, kutekeleza mageuzi ya kisheria, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya na kijamii huku zikichukuwa hatua za kuzilinda familia.

Kwa kufanya hivyo, alisema, “tunaweza kupunguza pakubwa hatari ya msichana kupokwa utoto wake kupitia ndoa za utotoni.

Chanzo: AFPESource link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *