Virusi vya corona: Athari ya biashara ya mitumba Afrika Mashiriki


Biashara ya mitumba Afrika Mashariki
Maelezo ya picha,

Biashara ya mitumba Afrika Mashariki

Wafanyabiashara wa nguo za mitumba nchini Kenya na Tanzania wametoa ombi kwa serikali zao kutopiga marufuku uagizaji wa bidhaa hizo kutoka ng’ambo, wakisema wako tayari kutekeleza mikakati ya kiusalama ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya Covid-19 kama vile kupiga dawa nguo hizo.

Biashara ya mitumba imedorora tangu Machi mwaka huu wakati maambukizi ya corona yalipoanza.

Kisha serikali ya Kenya ilipiga marufuku uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nchi za nje. Tanzania nayo ilisitisha safari za ndege kutoka ng’ambo hadi nchini humo mnano mwezi Aprili, lakini baadae serikali iliondoa marufuku hiyo.

”Biashara imekuwa ngumu kwasababu kuna baadhi ya watu waliokuwa na imani kuwa nguo za mitumba zinaleta ugonjwa wa corona, na wengine wakaacha kutembelea duka letu kabisa, ila sasa hali ni tofauti kwasababu hiyo hofu imepungua,” anasema Clement Andrew ambaye anamiliki duka la Mitumba Brand mjini Dar Es Salaam, Tanzania.

Wafanyabiashara wamelazimika kutafuta mbinu mpya za kuuza nguo zao hasa kupitia mitandao ya kidijitali.

”Huwa tunapiga picha nguo hizo kisha tunaziweka kwenye ukurasa wetu wa Instagram, na hii imevutia wateja kutoka maeneo ya nje ya Tanzania kama vile Nairobi na Mombasa nchini Kenya, Lilongwe nchini Malawi, na hata Zambia na Afrika Kusini,” anaelezea John Steveny Kimbali anayemiliki duka la Mitumba Brands mjini Dar Es Salaam.

Wafanyabiashara wanaotengeneza nguo zao wenyewe katika eneo la Afrika Mashariki wamekuwa wakishinikiza serikali zipige marufuku uagizaji wa mitumba ili kupanua sekta ya viwanda. Mmoja wao ni Robert Mtoto anayemiliki Mtoto Designs nchini Kenya.

”Nguo zetu saa hii zimeanza kutoshana bei na nguo za mitumba, lakini sisi ambao tunatengenezea nguo hapa Kenya hatuna uwezo wa kutengenezea kila mtu nguo. Soko lipo lakini mitumba inaharibu biashara, kama itafungiwa watu hawa watalazimika kununua nguo kuoka kwetu,” anasema Mtoto.

Maelezo ya picha,

Biashara ya mitumba Afrika Mashariki

Utafiti wa hivi karibuni wa Kituo cha Maswala ya Uchumi (IEA) unaonyesha kwamba sekta ya mitumba inawaajiri takribani watu milioni mbili nchini Kenya.

Chama cha wafanyabiashara wa nguo za mitumba nchini Kenya kimekuwa kikipinga vikali kuwekwa kwa marufuku ya kuagizia mitumba kutoka ng’ambo, kikidai kuwa hali ya maisha ya watu wengi itaathiriwa.

Katibu wa chama hicho Nancy Njoroge amesema kwamba mazungumzo yanaendelea baina yao na serikali kuhusu mikakati ya kuhakikisha kuwa biashara ya mitumba haisaidii kusambaza virusi vya corona.

”Serikali ya Kenya ilikuwa imependekeza tutoe mizigo ambayo iliwekwa kwa meli kabla ya tarehe 7 Aprili. Kisha ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zinapuliziwa dawa kabla ya kuondoka ng’ambo, na baada ya kufika humu nchini tuhakikishe tumepuliza bidhaa hizo dawa,” anasema Nancy.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *