Virusi vya corona: Utamaduni wa Wabukusu Kenya wa kupasha tohara ulivyoathirika na corona


Jamii ikisindikiza wanaokwenda kutahiriwa

Maelezo ya picha,

Jamii ikisindikiza wanaokwenda kutahiriwa

Jamii ya wabukusu kutoka magharibi mwa Kenya inatambulika kwa kufuata mila yao ya kutahiri watoto wa kiume.

Jamii hii ambayo ni mojawapo wa makabila 17 ya Waluhya, huwa na sherehe ya kipekee ambayo huvutia macho ya watu wengi kutokana na jinsi wanavyoendesha utamaduni huo.

Agosti mosi ndio siku ya kuanza kwa utamaduni huo ambapo shamra shamra huendelea kwa mwezi mzima.

Siku hiyo huanza kwa watoto wa ngariba watakaotoa huduma za kutahiri kwa jamii.

Sinino Omukongolo ni ngariba mkuu katika kaunti ya Bungoma.

Maelezo ya picha,

Sinino Omukongolo ni ngariba mkuu katika kaunti ya Bungoma

Amekuwa akifanya kazi hii kwa miaka nyingi.

“Siku ya kwanza, huwa tunawatahiri watoto wa ngariba ili kufungua njia ya kutahiri wengine. Hii ni hatua ya pili. Hatua ya kwanza ni kutakasa visu ambavyo hutumiwa kutahiri, na hii tunafanya siku chache kabla ya tarehe moja Agosti ”

Siku kuu, asubuhi na mapema baada ya jogoo kuwika, vijana hao huchukuliwa na kupelekwa kwenye mto ambapo huvuliwa nguo na kupakwa udongo mweupe mwili mzima.

Inaaminiwa kwamba udongo huo ni nguo ambayo itamsitiri hadi wakati atakapopona.

Maelezo ya picha,

Inaaminiwa kwamba udongo huo ni nguo ambayo itamsitiri hadi wakati atakapopona

“Kijana anapopakwa udongo, inamaanisha kwamba lazima atahiriwe, hakuna kurudi nyuma hata kutoke nini, jua haliwezi kutua kabla hajatahiriwa”, Omukongolo amesema.

Baada ya hilo, wanarejea nyumbani huku wakisindikizwa na nyimbo ambazo zingine ni za tangu jadi na zingine ambazo hutungwa kulingana na matukio ambayo yanaendelea.

Wimbo mmoja baada ya mwingine huimbwa huku hadhira ikicheza densi tofauti tofauti mtindo mkuu ukiwa ule wa kutingisha mabega unaojulikana kama isikuti wakielekea nyumbani kwa anayetahiriwa.

Wanapowasili nyumbani, mjomba humvalisha nyama ya ng’ombe aliyechinjwa shingoni.

Maelezo ya picha,

Kijana akilia wakati anatahiriwa ana aibisha ukoo

Punde baada ya kufanya hivyo, anampisha ngariba ambaye atamtahiri.

“Hiyo nyama huwa tunasema ni ya kuweka ukoo pamoja… Kijana hapaswi kulia, akifanya hivyo atakuwa anaaibisha ukoo”, Omukongolo amesema.

Nyumba moja baada ya nyingine, boma moja baada ya jingine, kijiji kimoja baada ya kingine shughuli huwa ni hii tu na hufanyika kutwa kucha kwa mwezi mzima.

Mwezi wa kumi, ngariba hurejea na wazee wengine na kuwashauri vijana waliotahiriwa. Msimu huu hukamilika mwezi wa Desemba wakati vijana wanapotoka jandoni.

Hata hivyo msimu huu hutumiwa pia kutabiri matukio ambayo yanakuja kutokea katika jamii.

Maelezo ya picha,

Wakati wa sherehe pia wanaweza kutabiri kitakachotokea siku za usoni

“Sisi ngariba huchinja kuku na mbuzi, wazazi wa watoto huchinja ng’ombe. Tunapotazama nyama, kuna jinsi ambavyo tunaweza kuona na kujua mambo ambayo yanatungoja katika miaka inayofuata. Kama kutakuwa na njaa, tukiangalia hiyo nyama ya ng’ombe tutaona… kama kutakuwa na shida za kisiasa tutajua… Tutaangalia nyama na tutajua”, Omukongolo amesema.

Ni utamaduni wa karne ya 17 ambao umekuwa ukirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine licha ya kunyooshewa kidole cha lawama kuhusu visu vinavyotumiwa kuonekana kwamba vinaweza kusababisha kusambaa kwa magonjwa ya kuambukiza.

Maelezo ya picha,

Jamii hii imeshindwa kuahirisha sherehe ya mwaka huu kwasababu ya uwezekano wa watu wengine wakubwa wakajipata kwenye rika la watoto

Nguvu ya mila

Mwaka huu kuzuizi kikubwa kimekuwa ugonjwa wa virusi vya corona, kwasababu utamaduni huo unachukuliwa kuwa wenye uwezekano mkubwa wa kusababisha maambukizi ya corona. Lakini nguvu ya mila, imefanya wenyeji kuona vigumu sana kuahirisha tukio la mwaka huu.

“Hatuwezi kuahirisha… Kuahirisha ina maana kwamba vijana wasitahiriwe, na hatua hiyo itaathiri rika la mwaka wa 2022. Utapata mtu ni mzee lakini yuko kwenye rika la watoto na hilo haliwezekani”, Omukongolo amesema.

Omukongolo anasisitiza kwamba wamechukua tahadhari wakati huu wa corona kwa kuzingatia masharti ya wizara ya afya.

“Sisi kila wakati huchukua tahadhari… Tuna sheria zetu wenyewe ambazo ni za kuwalinda wanaotahiriwa na pia jamii. Kwa mfano mtu ambaye ni chongo hawezi kuwa ngariba. Kwa hivyo pia wakati huu tunaelewa hali jinsi ilivyo ndiyo maana tunasema kila mtu avalie barakoa, na kukaa umbali wa mita 2. Hata watu watakaosindikiza vijana tumewaweka kwa makudi ya watu ishirini kinyume na awali”, Omukongolo amesema.

Mapema mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufuku mikusanyiko ya watu ikiwemo makanisani, mikutano ya kisiasa, na sherehe zozote kama njia moja ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Hata hivyo sheria hii inaonekana kuwa vigumu kuzingatiwa hasa wakati ambapo sherehe hizi zinaanza.

“Hizi sherehe zetu huvutia umati mkubwa wa watu na kwa kawaida huwa ni vigumu sana kudhibiti umati huo,.. Na wakati huu wa corona itatuletea madhara makubwa. Kwa hivyo tunawashauri watu wetu waende hospitalini. Kama vile tuliwashauri wasiende makanisani,” anasema Gavana wa Kaunti ya Bungoma Wycliffe Wangamati.

Iwapo masharti ya serikali ya kuahirisha sherehe hizi yatafuatwa ina maana kwamba sherehe nyengine kama hiyo itafanyika tena mwaka wa 2022.

Jamii ya Wabukusu hutahiri vijana wao kila baada ya miaka miwili na kuwaweka katika rika lao. Kwa jumla jamii hii ina makundi manane ya marika. Watakao tahiriwa mwaka huu watawekwa katika rika la ishirini la ‘Bakikwameti’ ishara tosha kwamba wametolewa ngozi ya mama na sasa wamekuwa wanaume kamili.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *