Waridi wa BBC: Wanaume huogopa kunitongoza wakisikia mimi ni bondia, asema Fatuma Zarika


fatuma Zarika

Fatuma Zarika ni mwanamke ambaye anajulikana sana katika Afrika ya mashariki na ya Kati, kutokana na ubabe wake katika ulingo wa ndondi licha ya kwamba sifa hizo anasema zimepokelewa tofauti.

Kwa mfano Zarika anasema kuwa wanaume wanaogopa kumtongoza kimapenzi. Anahisi kuwa wanamuona kama mtu asiyeweza kukaribiwa ovyoovyo, kutokana na kipaji chake cha ndondi. Zarika ni Mkenya wa kwanza kuwahi kushinda taji la baraza la ndondi duniani WBC katika uzani wa Super Bantam.

Na sio ajabu kwa wale ambao wamekuwa wakimtazama bingwa huyu wa masumbwi akiwa ulingoni kama mwanamke mwenye nguvu ajabu.

Ni mwanamke mwenye ukakamavu na sura iliyo tayari kupigania nafasi yake kama bingwa kwa hali na mali. Utapigwa na butwaa anavyoyarusha makonde kwa mpinzani wake.

Cha ajabu ni kuwa tofauti na jinsi Zarika anavyoonekana kwenye jukwaa, kama bondia hatari na moto wa kuotea mbali , katika maisha yake ya uhalisia ni mtu wa kawaida tu.

Maelezo ya picha,

fatuma zarika akitangazwa mshindi wa taji la WBC jijini Nairobi

Fatuma Zarika, ambaye sasa ana miaka 38, ni mama wa mabinti wawili wa miaka 23 na 21. Maisha yake yote anasema ameishi kuhakikisha kuwa anatoa maisha bora na nafasi za kujiimarisha maishani kwa mabinti wake.

Malezi ya Zarika

Haya ni tofauti na maisha ya utotoni ya bingwa huyu. Fatuma alizaliwa katika mtaa mmoja wa mabanda jijini Nairobi na maisha yake ya utotoni yalikumbwa na uchochole wa aina yake.

Mamake kwa jina Aisha Musa alikuwa ni mama mlezi wa kipekee aliyekuwa na jukumu la kumlea Fatuma na ndugu yake Hemed Musa.

Maelezo ya picha,

fatuma Zarika akisimama na wadhamini pamoja na waandalizi wa pigano la uzani wa bantam jijini Nairobi

Ni maisha yaliokuwa magumu sana na ilimlazimu Fatuma kuanza kutafuta fedha akiwa bado mdogo ilimradi kusaidiana na mamake katika familia yao.

Baada ya kumaliza masomo ya shule ya msingi, Zarika hakuweza kujiunga na shule ya sekondari kwa kukosa karo.

Badala yake alishirikiana na mamake kuhakikisha kuwa nduguye mdogo angepata masomo.

Kufanya kazi kama yaya

Kazi aliyoipata ilikuwa ya yaya ambapo alifanya kazi kwa miaka mitatu.

“Kila mwaka nilifanya kazi katika nyumba tofauti. Nilikuwa najiambia afadhali niwe kijakazi kuliko kufanya matendo mabaya ili kupata fedha. Ni afadhali nifue nguo za watu kuliko kuchukua mkondo mbaya wa maisha,” Zarika anasema.

Kutafuta maisha kupitia Michezo

Baada ya muda, Zarika aliamua kujaribu kusakata soka. Lakini baada ya muda mfupi tu, aligundua kuwa haikuwa kwenye damu yake na hapo ndipo akageukia ndondi.

Aliendelea kufanya mazoezi na kujituma hata zaidi ili awe mwanabondia hodari. Kwa kuendelea kufanya hivyo aligundua kuwa moyo wake ulikuwa kwenye ndondi

Mwaka wa 2000 alishindania taji katika kiwango cha eneo alilokuwa anaishi. Wakati huo alipigana na mwanamke aliyekuwa gerezani na bado anakumbuka alivyopigwa kichapo cha ajabu.

Maelezo ya picha,

Fatuma Zatrika akiwa Dubai anakofanya kazi

Licha ya hayo aliamua kuendelea kujinoa na kuwa bora zaidi.

Hakukata tamaa baada ya kushindwa mara ya kwanza kwani alianza kuwa na kiu cha kufanikiwa.

Zarika pia anasema kuwa kutokana na maisha ya shida aliyokuwa nayo alikuwa anatafuta jinsi ya kupitisha wakati ili asizongwe na mawazo kutokana na matatizo yaliokuwa yakimkodolea macho.

Mwaka wa 2016 Zarika alivunja rekodi kwa kuwa Mkenya wa kwanza kushinda taji la Super Bantamweight mara tatu.

Ili kuhifadhi ubingwa huo, Zarika alilazimika kupitia makubwa, Alipigana mapigano matatu makuu.

Mwaka 2018, alikumbana na ushindani mkali kutoka kwa raia wa Mexico Yamileth Mercado.

Alipambana pia dhidi ya Mzambia Catherine Phiri mwaka wa 2017 na 2019.

Katika mapigano hayo yote Fatuma Zarika ameibuka na ushindi mkubwa .

“Haijakuwa rahisi kwangu kutwaa ushindi wa namna hii. Nimejituma sana katika kazi hii. Ningeomba sana mataji kama haya pia yaandamane na malipo sawia na sifa na umaarufu unaotokana na ushindi wa namna hii,” anasema Zarika.

Pia Zarika anajionea fahari ya kusafiri hadi Uingereza na kufanya mazoezi na wanamieleka wakubwa duniani.

Huo ni mwaka wa 2017 alipopata fursa ya kufanya mazoezi na waliokuwa mabingwa kwa mfano bingwa wa Cruiserweight Tony Bellew

Maisha yake kama mwanamke yamekuwaje?

Maelezo ya picha,

fatuma zarika katika pigano lake la raia wa Zambia Phiri ambapo alifanikiwa kutetea taji lake la WBC

Zarika hajafanikiwa kwa sasa kufunga ndoa.

Anasema kuwa ‘kila kitu na wakati wake’ na kwa sasa ndoa haimo akilini mwake kwani kuna mambo mengine muhimu anayoyafuata maishani.

Hapo awali Zarika alikuwa na uhusiano na mwanamume ambaye ni baba wa watoto wake wawili.

Ndoa zinapandashuka zake na anaamini kuwa uhusiano wao haukufanikiwa na ilikuwa vyema kwamba waliachana. Zarika alibaki kuwalea watoto.

Kila siku Zarika anasema kuwa mabinti wake ndio sababu kubwa ya yeye kuwa na nguvu ya kuendelea kuishi.

“Hawa wanangu wamekuwa nguzo kuu maishani mwangu. Ndio kiini kikubwa cha mimi kuamua kuingia kwenye masumbwi, kwa kuwa sikutaka wakose kusoma,”alisema Zarika.

Siwezi kutaka wanangu waniige

Zarika anasema kuwa hawezi kutamani mabinti wake kujitosa kwenye ulimwengu wa ndondi.

Maelezo ya picha,

fatuma zarika akiwa na wanawe wawili wa kike

Anasema kuwa sio ulimwengu wa raha na starehe.

Anasema mchezo huo unahitaji mtu kuwa sugu na mtu ambaye hakati tamaa haraka.

“Kuna faida na hasara pia,” anasema, na kutaja mfano kwamba amewahi kupata majeraha mabaya mno.

“Niliumizwa vibaya usoni mwangu na ni kawa nina matatizo ya kuona vizuri. Huwa naogopa ninaweza kuumia na kupooza lakini mimi huamini Mungu hunilinda nikiwa kwenye ulingo wa masumbwi,” anasema Zarika.

Fatuma Zarika kwa sasa anaishi Dubai ambako anafanya kazi ya kuwafanyisha watu mazoezi na hivyo ndivyo anavyojipatia riziki yake.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *