Washiriki wa mdahalo wa chama cha Demokrat watofautiana juu ya biashara, afya na sera za kigeniJumla ya Wademokrat sita wanaogombea walitofautiana juu ya masuala ya biashara, huduma ya afya na sera ya kigeni.

Na kulikuwa na ukosoaji mwingi dhidi ya Rais Donald Trump na mvutano wa hivi karibuni na Iran.

Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden

Joe Biden, mgombea kwa tiketi ya Wademokrat alisema : “Tumepoteza heshima yetu katika eneo hilo. Tumepoteza ushirikiano na washirika wetu. Rais anayekuja ni lazima awe na uwezo kuwaleta washirika wetu pamoja.”

Biden alikosolewa na Seneta wa Vermont Bernie Sanders juu ya kuunga kwake mkono vita vya Iraq.

Na Sanders alisema anahofia mvutano ulioko kati ya Marekani na Iran unaweza kuelekea pabaya.

Sanders alisema : “ Na hivi sasa kile kinachonitia wasiwasi kabisa ni tunaye rais ambaye anasema uongo tena na anaweza kutuingiza katika vita ambayo itakuwa mbaya kuliko ile ya Iraq.

Wasiwasi huo huo ulielezwa na aliyekuwa meya wa South Bend, Indiana na mstaafu wa vita Pete Buttigieg.

Buttigieg : “Tunaweza kuendelea kupambana bila ya kuwa na majeshi ya kudumu ardhini. Lakini kile kinachoendelea hivi sasa ni kuwa rais anatuma majeshi zaidi.”

Suala la vikosi vya Marekani

Baadhi ya wagombea wanataka kupunguza vikosi vya Marekani katika Mashariki ya Kati na Seneta wa Massachusetts Elizabeth Warren anasema ni wakati muwafaka kuondoa vijeshi vya Marekani kutoka Afghanistan.

Warren alisema : “Hakuna mtu aliyekuwa na suluhisho na utatuzi wa kulimaliza hili. Ni lazima tuondoshe vikosi vyetu huko. Havisaidii kuweka mazingira salama zaidi kwa taifa la Marekani au eneo hilo.”

Bilioneya na mwanasiasa mpya

Kwa upande wa bilioneya na mwanasiasa mpya Tom Steyer, ni wakati wa kuanza kushughulikia upya usalama wa taifa.

Steyer alisema: “Siyo suala zaidi la uzoefu, ni suala la kukata shauri. Iwapo umekuwa unasikiliza suala hili, kile tunachosikia ni miaka 20 ya makosa yaliyofanywa na serikali, Mashariki ya Kati.

Wademokrat walivutana juu ya nani kati yao ni mwenye maandalizi bora ya kumshinda Rais Trump katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.

Warren alijaribu kuondoa fikra ya kuwa mgombea mwanamke atakuwa dhaifu katika kinyang’anyiro hicho.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *