WHO: Hakuna haja ya kuwa na hofu ya virusi vya Corona


Akizungumza Jumtatu na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Italia, Roma, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani barani Ulaya, Hans Kluge amewatoa hofu wananchi, akisema kiwango cha vifo ni asilimia mbili na kwa sasa asilimia moja iko nchini China, ambako kuna asilimia 96.5 ya visa vyote duniani.

”Ningependa kurudia ujumbe wangu kwamba hakuna haja ya kuwa na hofu yoyote. Ni kweli naelewa watu wana wasiwasi kuhusu afya zao na afya za familia zao. Idadi ya visa China inapungua, tunaishukuru serikali ya China kwa kuchukua hatua madhubuti. Asilimia 80 ya wagonjwa wana dalili ndogo na wengine wamepona, asilimia 5 wako katika hali mbaya na asilimia 2 wamekufa, lakini wengi wao ni wazee wenye kinga hafifu,” alifafanua Kluge.

Kluge amebainisha kuwa watu 12 wamekufa Italia, wote wakiwa wazee na mwanaume mmoja raia wa Ufaransa ambaye amefariki katika hospitali moja mjini Paris usiku wa kuamkia leo alikuwa na umri wa miaka 60. Hata hivyo inaaminika kuwa mwanaume huyo kutoka mji wa Crepy-en-Valois hakusafiri kwenda kwenye eneo lolote lile lililotambuliwa kuathirika na virusi vya Corona.

Schweiz WHO Coronavirus Covid-19 (picture-alliance/dpa/S. di Nolfi)

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema idadi ya visa vipya vilivyoripotiwa jana Jumanne nje ya China ni zaidi kuliko vile vya ndani ya China, hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu virusi vya COVID-19 vilipozuka. Italia imekuwa ikijaribu kutuliza wasiwasi uliopo

na imeomba msaada wa kimataifa katika juhudi zake za kukabiliana na virusi vya Corona huku ikiwa na wagonjwa 374.

Wakati huo huo, kituo cha televisheni cha Ujerumani, WDR kimeripoti kuwa mke wa mgonjwa aliyeambukizwa virusi vya Corona ambaye yuko mahututi katika hospitali ya Duesseldorf, naye pia ameathirika na virusi hivyo. Kwa mujibu wa taarifa hizo, huenda mwanamke huyo alikuwa akifanya kazi katika shule ya chekechea.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa ataitisha mkutano na waandishi habari siku ya Jumatatu kuzungumzia virusi vya Corona, wakati ambapo ugonjwa huo ukizidi kusambaa ulimwenguni.

Algeria nayo imesema haina mpango wa kuzuia maandamano ya umma au kusitisha safari za ndege kwenda Italia, baada ya nchi hiyo kuripoti kisa cha kwanza cha Corona kwa mwanamme ambaye ni raia wa Italia. Mkurugenzi wa kuzuia na kupambana na magonjwa ya kuambukizi nchini Algeria, Djamel Fouar amesema maafisa wanawafuatilia kwa karibu watu wote waliokuwa na mawasiliano na mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 61.

(AP, DPA, Reuters)

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *