Afrika Kusini yarejesha vizuizi vikali vya Covid-19


Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, alisema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, kwamba visa vya maambukizi ya Covid-19 nchini humo ndani ya siku saba zilizopita vilikuwa juu kwa asilimia 31 zaidi ya wiki iliyotangulia, na asilimia 66 zaidi ya wiki ya kabla. Ramaphosa alitangaza Jumapili kwamba baadhi ya maeneo nchini humo ikiwemo jiji la kibiashara la Johannesburg na mji mkuu wa Pretoria yanakabiliwa na wimbi la tatu la Covid-19.

“Wakati nchi ikielekea kwenye wimbi la tatu la maambukizi, bado hatujui litakuwa kali kiasi gani na litadumu kwa muda gani. Kulingana na ushauri wa wanasayansi kwa serikali, ukali wa wimbi la tatu utategemea na kiwango cha watu kutangamana. Hii inamaanisha kila mmoja anahitaji kufikiria juu ya watu anaowasiliana nao kila siku na kufanya kila awezalo kupunguza mawasiliano hayo”, alisema Rais Ramaphosa.

Wakati Afrika Kusini ikirejesha vizuizi vikali, Kenya nayo kupitia wizara ya mambo ya ndani imetangaza kurefusha marufuku ya kutotoka nje usiku kwa siku nyingine 60 ili kukabiliana na maambukizi. Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa rais Uhuru Kenyatta alioutoa mwishoni mwa mwezi machi wa kurefusha marufuku hiyo kuanzia saa nne usiku hadi 10 alfajiri.

Ghana Covax

Chanjo za Covid-19 kupitia mpango wa CoVAX

Kwingineko afrika, Burkina Faso imepokea shehena ya kwanza ya dozi 115,200 za chanjo ya Covid 19, kupitia mpango wa kimataifa wa usambazaji chanjo katika mataifa maskini wa COVAX. Wizara ya afya nchini humo imesema zoezi la utoaji chanjo litaanza na watu walio katika hatari wakiwemo wahudumu wa afya na mahujaji wanaotakiwa kwenda mjini Mecca.

Hapa barani Ulaya Ufaransa kuanzia Jumatatu imefungua milango ya utoaji chanjo kwa watu wazima wote, ikiwa ni wiki moja kabla ya Ujerumani kufanya hivyo ili kuepuka wimbi jingine la tatu la maambukizi yanayotokana na aina mpya ya kirusi.

Hadi sasa watu milioni 25.4 nchini Ufaransa wamepatiwa dozi ya kwanza ya chanjo ambayo ni sawa na asilimia 38 ya idadi jumla ya watu.

Wakati huohuo waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn anakutana na mawaziri wenzake wa majimbo yote 16 kujadili njia za udhibiti wa vituo vya kupima kufuatia kashfa ya udanganyifu. Tangu kuwepo na madai ya visa vya udaganyifu, waziri Spahn alisema kwamba kutakuwepo na hatua kali za udhibiti ingawa mjadala umeibuka wa jinsi gani ya kuvithibiti vituo vya upimaji na nani anapaswa kuvishughulikia.

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *