Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa laridhia maazimio kuhusu Darfur na Sudan kusini


Kufuatia janga la corona kwa mara ya kwanza mataifa wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa  Mataifa kwa pamoja yameridhia maazimio manne kwa njia ya barua pepe. Wanadiplomasia wa nchi hizo wamepigia kura azimio la kuendelea kusalia kwa wanajeshi wa umoja huo katika jimbo la Darful nchini Sudan hadi mwishoni mwa mwezi Mei. Na kuendeleza mpango wa kufanikisha ustawi wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia hadi Juni 30. 

Aidha wamerefusha muda wa mamlaka ya jopo la wataalam linalofuatilia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini hadi Aprili 30, 2021. Na mwisho wamesisitiza  umuhimu wa kuunga mkono shughuli za ulinzi wa amani katika maeneo tofauti ya ulimwengu.

Mkutano umetokana na hofu ya COVID-19

Chombo hicho chenye nguvu kubwa kabisa cha Umoja wa Mataifa kimefanya mkutano kwa njia ya video kutokana na adha ya ugonjwa wa COVID-19, ambao umelivuruga vibaya jiji la New York, ambako Umoja wa Mataifa una makao makuu yake. Mkutano wa mwisho wa baraza hilo kufanyika katika makao makuu hayo ulikuwa Machi 12, ambapo azimio la kuridhiwa kurefushwa mamlaka ya mpango wa ulinzi wa amani wa Sudan Kusini na kuhamasisha maendeleo kuelekea amani ya taifa hilo changa barani Afrika. Azimio lililodhaminiwa na Uingereza pamoja na Ujerumani linarefusha jitihada ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ya jeshi la ulinzi wa amani linalojulikana kama UNAMID hadi Mei 31, pale ambapo baraza hilo limesema litaamua namna ya kuondoka kwa ujumbe huo wa kijeshi jimboni Darfur.

Chanzo cha vurugu ni mgogoro wa Darful

Mgogoro wa Darful ulianza 2003 pale kundi la waasi kutoka jamii ya weusi, kuwatuhumu wanamgambo wa  Kiarabu katika serikali za Sudan kufanya vitendo vya ukandamizaji dhidi yao. Serikali ya Sudan ililaumiwa kwa kufanya kitendo cha kulipiza kisasi kwa kuipa silaha jamii ya wafugaji ya Kiarabu ili kuiangamiza jamii hiyo ya weusi, madai ambayo hata hivyo, serikali imeyakanusha.

Kumekuwa na shinikizo, likiwemo la kutoka kwa Rais Donald Trump wa Marekani, kupunguza idadi ya wanajeshi wa UNAMID, kwa lengo la kupunguza mapigano na kuweka mazingira ya usalama. Jeshi hilo lililoanzishwa 2007 ni moja katika mpango ghali sana wa amani wa Umoja wa Maataifa, likijumisha wanajeshi 15,845 na polisi 3,403.

Julai 2018, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipigia kura azimio la kupunguza ukubwa  wa ujumbe huo, ambapo lengo lilikuwa kumaliza kabisa operesheni hiyo ifikapo Juni 30,2020. Lakini maandamano ya umma ambayo yalianza mwishoni mwa mwaka 2018 na kufanikisha kuondolewa madarakani rais wa zamani wa Sudan Omar Al-Bashir na baadae kuunda kwa serikali ya mpito, vyote kwa pamoja vilisababisha kucheleweshwa kufanikishwa kwa uamuzi huo.

Mpaka Januari UNAMID ilikuwa na wanajeshi zaidi ya 4,300, polisi wa kimataifa zaidi ya 2,100 na wafanyakazi wa kiraia 1,500.

 Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *