Biden na Harris kumenyana mdahalo wa pili wa Democratic


Katika usiku wa pili wa midahalo ya wagombea wa chama cha Democratic, Biden atakuwa jukwani pamoja na Harris na Cory Booker, ambao ni maseneta na wagombea mashuhuri zaidi wenye asili ya kiafrika katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa chama cha Democratic ambamo suala la rangi limekuwa na mchango mkubwa.

Wagombea wengine saba, akiwemo waziri wa zamani wa makaazi Julian Castro, Gavana wa Washington Jay Inslee na Seneta mwingine Kirsten Gilibrand, watanungana nao jukwani mjini Detroit katika mdahalo unaotazamiwa kuleta kasi mpya katika kampeni zao.

Usiku wa Jumanne, maseneta Berni Sanders na Elizabeth Warren walitetea mara kwa mara mapendekezo yao ya mageuzi chini ya ukosoaji mkubwa kutoka wapinzani wao wenye msimamo wa wastani waliohoji kwamba mipango yao ya kutoa huduma za afya kwa wote, kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuhalalisha uvukaji wa mipaka kinyume cha sheria, ingewawumiza Wademocrat kwenye uchaguzi mwakani.

CNN Demokratische Debatte in Detroit (picture-alliance/newscom/E. M. PioRoda)

Maseneta Bernie Sanders na Elizabeth Warren wakiwa katika mdahalo mjini Detroit Julai 30, 2019.

“Tunahitaji usalama wa mpakani, na tunaweza kufanya hilo. Lakini kile ambacho hatuwezi kufanya ni kuacha maadili yetu. Nimekuwa mpakani. Nimewaona kina mama, nimeona vizimba vya watoto. Tunapaswa kuwa nchi ambayo, kila siku, inaheshimu maadili yetu. Na hilo linamaanisha, hatuwezi kukigeuza uhalifu, kitendo cha mtu kuja hapa,” alisema Seneta Elizabeth Warren.

Kundi hilo la wagombea karibu dazeni mbili limekuwa likiwania nadhari na msaada wa kifedha katika kinyanganyiro cha chama cha Democratic ili kuchagua mpinzani wa Trump katika uchaguzi wa Novemba 2020.

Biden akiri kushtushwa na mashambulizi ya Kamala

Biden hakuonekana sana kwenye usiku wa kwanza wa mdahalo lakini kuna uwezekano mkubwa akawa kivutio cha usiku wa pili. Makamu huyo wa zamani wa rais amekuwa katika malumbano kwa wiki kadhaa na Seneta Harris na Booker kutafuta kura za jamii ya wapigakura wenye asili ya Afrika, ambao ni sehemu muhimu ya kinyang’anyiro cha uteuzi wa chama cha Democratic.

Biden alikiri kushangazwa mwezi uliopita wakati Harrison alipomkosa kwa kupinga mpango ulioidhinishwa na serikali kuu kwa shule katika miaka ya 1970, na kwa kushirikiana na makundi ya wabaguzi wakati akihudumu katika baraza la seneti miongoni kadhaa iliyopita.

USA, Washington: Einf├╝hrung des Gleichstellungsgesetzes (Reuters/L. Millis)

Seneta Cory Booker.

Mashambulizi hayo makali yalimuongezea umaarufu Harris kwenye maoni ya wapigakura, na majibu yasioridhisha ya Biden yalipunguza umaarufu wake. Lakini amerejesha umaarufu huo kulingana na uchunguzi wa karibuni na bado anashikilia nafasi ya kwanza ya uungwaji mkono miongoni mwa wapigakura wenye asili ya Afrika.

Booker, aliekuwa jukwani pamoja na Biden katika mdahalo uliopita, ameongeza mashambulizi yake, akimtaja kuwa mwasisi wa mpango wa kuwatia gerezani watu wengi wakati wa mkutano mjini Detroit wiki iliyopita, akimaanisha kazi ya Biden kama Seneta kuhusu muswada wa uhalifu wa mwaka 1994, ambao wakosoaji wanasema ulisababisha ufungwaji wa wanaume wengi wenye asili ya Afrika.

Biden na kampeni yake walijibu kwa kukosoa kipindi cha Booker kama meya wa Newark, New Jersey, ambako aliongoza idara ya polisi ambayo baadae ailikuja kuchunguzwa kwa ukiukaji wahaki za kiraia.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,rtrtv

Mhariri: Sekione KitojoSource link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *