Polisi nchini Sudan wawatawanya waandamanaji


Waandamanaji wamefurushwa kwa gesi ya kutoa machozi

Haki miliki ya picha
Getty Images

Polisi nchini Sudan wamewasambaratisha waandamanaji kwa gesi ya kutoa machozi walipoingia barabarani wakishinikiza kukoma kwa utawala wa kijeshi mjini Khartoum.

Maelfu ya waandamanaji walikuwa wakiimba ”utawala wa kiraia” polisi walipowatawanya kwenye maeneo kadhaa ya mji wa Khartoum, mashuhuda wameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP.

Siku ya Jumamosi, vikosi vya kijeshi vilivunja mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na waratibu wa maandamano.

Jeshi nchini humo lilimuondoa madarakani rais Omar al-Bashir mwezi Aprili.

Bashir aliingia madarakani kwa mapinduzi tarehe 30 mwezi Juni mwaka 1989.

Wanaharakati waliitisha maandamano siku ya Jumapili, maandamano ya kwanza yaliyopangwa tangu watu kadhaa walipouawa baada ya jeshi kushambulia waandamanaji tarehe 3 mwezi Juni.

Maelfu ya watu waliandamana kwenye miji mbalimbali nchini Sudani kutaka mabadiliko ya utawala na kukabidhiwa kwa raia.

Jeshi lawakamata viongozi wa upinzani Sudan

Omar Al Bashir ashtakiwa

Mjini Khartoum, polisi waliwamwagia waandamanaji gesi ya kutoa machozi katika eneo la Bari, Mamura na Arkweit upande wa mashariki. AFP walikariri mashuhuda wa tukio hilo.

Maduka yalifungwa katika maeneo ambayo maandamano yalifanyika.

Vikosi vya usalama vilisambazwa katika maeneo mbalimbali kabla ya maandamano hayo.

Haki miliki ya picha
AFP

Kiongozi wa maandamano, Ahmed al-Rabie ameliambia shirika la AFP kuwa jeshi limevunja mkutano na waandishi wa habari mjini Khartoum siku ya Jumamosi.

”Kabla ya kuanza mkutano, magari matatu ya jeshi yakiwa na wanajeshi waliokuwa na silaha, walifika kwenye jengo letu.Walituambia tusifanye mkutano,” alieleza.

Kila mtu kwenye jengo alitakiwa kuondoka, alieleza bwana Rabie.

Aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa uvamizi uliofanywa ni ”ukiukwaji wa uhuru, na kitendo hicho ni kibaya zaidi kuliko utawala wa rais aliyepita.”

Jeshi lilisema litawawajibisha wapinzani ikiwa kutakuwa na machafuko au vifo wakati wa maandamano.

Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ajulikanaye kwa jina la Hemeti, amewaonya ”wahalifu” ambao watatumia vurugu hizo kutekeleza azma yao.

Mazungumzo kati ya baraza la mpito la kijeshi na upinzani yalivunjika baada ya tarehe 3 mwezi Juni na hayajafanyika tena pamoja na kuwepo kwa mpatanishi kutoka umoja wa Afrika na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

Siku ya Ijumaa, kuliripotiwa kuwa viongozi wa upinzani, walikamatwa na kushikiliwa huku jumuia ya kimataifa ikiombwa kushinikiza kuachiliwa kwao.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *