Tanzania: Waziri wa maliasili aonywa na rais


Rais wa Tanzania, John Magufuli

Haki miliki ya picha
Getty Images

Image caption

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa angalizo la muda wa siku 5 kwa waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Adolf Faustine Mkenda kuondoa tofauti zao katika kazi vinginevyo atatengua uteuzi wao.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 31 Desemba, 2019 alipokuwa akizungumza na maafisa na Askari wanyamapori na hifadhi ya misitu wa hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo ambako ametembelea na kujionea vivutio vya utalii.

Image caption

Waziri wa maliasili na utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla

Pamoja na angalizo hilo rais Magufuli ametoa pongezi kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kazi nzuri ya uhifadhi, kukuza utalii na kuchangia mapato ya Serikali lakini ameelezea kusikitishwa kwake na mahusiano mabaya yaliyopo kati ya waziri Dkt. Kigwangalla na Katibu Mkuu wake Prof. Mkenda hali ambayo inasababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua.

“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, Katibu mkuu na waziri kila siku wanagombana na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu mkuu awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa, hilo ni lazima nilizungumze kwa dhati, siwezi kuwa na watendaji wa kuteua mimi halafu kila siku wanagombana, kuna mambo mengi hayaendi.”

Haki miliki ya picha
Getty Images

Rais Magufuli amesema Tanzania yenye Hifadhi za Taifa 22, imetoa zaidi ya asilimia 32.5 ya eneo la ardhi yake kwa ajili ya hifadhi na kwamba imefanya hivyo kwa maslahi ya watanzania na watu wote duniani wanaotembelea hifadhi hizo.

Ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kununua kivuko chenye uwezo wa kuchukua watu 100 na magari 4 ili kurahisisha usafirishaji wa watalii wanaoingia na kutoka katika hifadhi ya Taifa ya Rubondo wakiwa na magari yao.

Haki miliki ya picha
Getty Images

Vilevile rais Magufuli amesema kwa sasa Tanzania ina bustani za wanyamapori yaani zoo 23, mashamba ya wanyama 20 na ranchi 6 na ametoa wito kwa watanzania wakiwemo wastaafu katika tasnia ya wanyamapori kujitokeza kuanzisha bustani za wanyamapori, mashamba ya wanyama na ranchi ambazo zitasaidia kuvutia watalii na kuongeza kipato.

Mkuu wa hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo Kamishna Msaidizi Mofulu amesema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 456.6 inao wanyama mbalimbali wakiwemo Sokwe, Pongwe, Swala, Tembo, Twiga na pia ni mazalia ya samaki wa ziwa Victoria na ndege mbalimbali.

Kipindi cha kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2018/19 idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeongezeka hadi kufikia 5,700 kwa mwaka, walioingiza shilingi Bilioni 1.4 katika pato la Taifa.

Rais Magufuli amekuwa Rais wa kwanza kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo akiwa madarakani.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *