Virginia Beach: Watu 11 wameuawa kwa kupigwa risasi katika jumba la serikali Marekani


Photograph of the building where shooting occurred Picha ya jumba ambalo kisa hicho kilitokea

Haki miliki ya picha
Reuters

Image caption

Ufyatulianaji huo wa risasi ulifanyika katika jumba la serikali mjini humo.

Watu 11 wameuawa na wengine sita kujeruhiwa katika ufyatulianaji wa risasi uliofanyika katika jumba la serikali katika jimbo la Virginia nchini Marekani, polisi wamesema.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa mshukiwa ambaye ni mfanyakazi wa muda mrefu katika kituo cha manispaa ya Virginia , alifyatua risasi kiholela .

Mshukiwa huyo ambaye hakutajwa aliuawa baada ya polisi kuwasili katika eneo hilo na kumkabili.

Ripoti za ufyatulianaji huo wa risasi zilianza muda mfupi baada ya mwendo wa saa kumi Ijumaa.

Afisa mkuu wa polisi James Cervera alisema kuwa mtu huyo aliuawa baada ya maafisa wa polisi kumpiga risasi.

”Afisa mmoja wa polisi ni miongoni mwa wale waliojeruhiwa baada ya risasi kupiga nguo yake ya kuzuia risasi”, alisema afisa Cervera.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa wanaamini kwamba mshambuliaji huyo alikuwa peke yake. Lengo la mtu huyo bado halijatambuliwa.

Eneo la kandokando ya jumba hilo, lenye majumba mengi ya serikali lilifungwa na wafanyikazi wa serikali kuondolewa.

”Tuliwasikia watu wakipiga makelele, wakiwataka watu kutoka ndani ya majumba hayo ”, Megan Banton , msaidizi mmoja katika jumba hilo aliambia kituo kimoja cha runinga kwa jina WAVY.

“Haya ni maafa mabaya kwa wakaazi wa Virginia beach” , alisema gavana wa Virginia Ralph Northam katika mtandao wa Twitter.

”Moyo wangu unawalilia waathiriwa wa shambulio hilo na wale wote waliowapenda. Naelekea Virginia Beach kwa sasa na nitawasili katika kipindi cha saa moja baadaye”.

Meya wa Virginia Beach Bobby Dyer alielezea tukio hilo kuwa baya zaidi katika historia ya mji huo.

Maafisa wa Ujasusi wa FBI walikuwa katika eneo hilo kuwasaidia maafisa wa serikali za mtaa kuchunguza shambulio hilo kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.

Kulingana na mtandao wa Marekani wa Gun Violence Archive hili ni shambulio la 150 kufanyika nchini Marekani mwaka huu.Source link

Author: mas

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *